Na Mate Tongola Wakfu wa Keroche utatumia kima cha shilingi milioni hamsini mwaka huu kufanikisha mpango wa kuwapa mafunzo viongozi tisa watakaowahamasisha wafanyabiashara wadogo wadogo nchini. Afisa Mkuu Mtendaji wa Wakfu huo, Njoki Karuoya amesema mradi huo unalenga kuwapa motisha pamoja na mafunzo wafanyabiashara hao na kwamba utaenezwa kwenye pembe mbalimbali barani Afrika. Akizungumza wakati wa mkutano na Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Standard Group, Sam Shollei, Karuoya amesema viongozi hao watakutana na wasimamizi wa biashara, washauri pamoja na wataalamu wenye tajriba katika masuala hayo. Kwa upande wake, Shollei amepongeza hatua za wakfu huo akisema wakati umefika kwa vijana kujihusisha katika biashara mbalimbali ikizingatiwa kuwa nafasi za ajira zimepungua mno nchini.