Na, Suleiman Yeri
Mahakama ya Milimani siku ya Jumatatu imeahirisha kusikilizwa kwa kesi ya uchochezi dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi, SONU Babu Owino hadi tarehe 15 Oktoba. Hakimu Mkuu wa Mahakama hiyo, Kennedy Cheruiyot ameiahirisha kesi hiyo baada ya upande wa mashtaka kusema mashahidi wake wakuu wasingeweza kufika mahakamani leo hii. Wakati uo huo, Wakili wa Owino amesema hakuwa tayari kuendelea na kesi hiyo kwa vile hajapokea nakala muhimu kutoka upande wa mashtaka zikiwamo taarifa za mashahidi. Inadaiwa kuwa mnamo Juni 13 mwaka huu, katika Makao Makuu ya Chama cha ODM, Owino alitoa matamshi ya chuki dhidi ya Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria. Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu shilingi laki moja au bondi ya shilingi laki tano akisubiri kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi dhidi yake.