Na Mate Tongola

NAIROBI, KENYA, WANAFUNZI, Walimu na yeyote atakayepatikana na hatia ya kuiba mitihani ya kitaifa atakabiliwa na adhabu kali ikiwemo kuhudumu kifungo kirefu gerezani.

Iwapo wabunge wataupitisha mswada wa Mitihani ya Kitaifa wa mwaka elfu mbili kumi na sita uliowasilishwa bungeni na Mbunge wa Sabatia Alfred Agoi, watakaopatikana na hatia watahukumiwa kifungu cha miaka mitano gerezani au kulipa faini isiyozidi shilingi milioni tano.

Kwa mujibu wa mwaasisi wa mswada huo, iwapo utapitishwa na kuwa sheria, utachangia pakubwa katika kuleta nidhamu shuleni ikiwemo kudumisha nidhamu katika taasisi za elimu.

Itakumbukwa kuw amwezi Machi mwaka huu, Waziri wa Elimu Fred Matiang'i alivunjilia mbali bodi ya Baraza kKuu la Mitihani ya Kitaifa, KNEC na kuagizwa kuchunguzwa kwa wafanyakazi wa baraza hilo akiwemo aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji Joseph Kivilu.