Na, Stephen Mukangai

MAAFISA wa kupambana na matumizi ya dawa haramu miongoni mwa wanariadha kutoka Uingereza, watazuru taifa la Kenya baada ya ufichuzi wa shirika la habari la Ujerumani kuthibitisha kuwa matumizi ya dawa hizo haramu bado yapo katika kambi moja ya riadha humu nchini.  SHIRIKA la habari la ARD nchini Ujerumani siku ya Jumamosi lilipeperusha makala ambayo yalionesha madaktari wa Kenya wakiwapa wanariadha husika dawa hizo  kinyume cha sheria. 

HAYA yanajiri baada ya Kenya kupitisha sheria kali ya kupambana na kuenea kwa matumizi ya dawa hizo haramu.  VILEVILE ufichuzi huo umebaini kuwa madaktari hao huwapa dawa haramu wanariadha kutoka Uingereza ambao hufanyia mazoezi humu nchini. 

KATIKA video hiyo ya dakika nane iliyopeperushwa na runinga ya taifa la Ujerumani, mwandishi mpekuzi aliyejifanya kuwa kocha wa riadha na wakala waliokuwa wamevaa kamera za siri walifaulu kununua dawa hizo za kuongeza nguvu mwilini. 

SERIKALI ya Kenya kwa upande wake imesema inafanya uchunguzi wa kina kabla ya kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika.