Mshukiwa mmoja wa ugaidi amekamatwa akihusishwa na utegaji wa bomu lililosababisha vifo vya watu kumi na watatu katika Kaunti ya Mandera.

Kamanda wa Polisi wa Kaskazini Mashariki anayeondoka, Bunei Rono amesema wakazi walimnasa mshukiwa akijaribu kutoroka kisha kumwasilisha katika kituo cha polisi.

Mshukiwa amewaambia polisi kuwa yeye ni miongoni mwa watu sita waliotega bomu hilo aridhini na kwamba walikuwa na bunduki walizotumia kutekeleza shambulio hilo. Bunei amesema mshukiwa angali anahojiwa na tayari polisi wametumwa kuwatafuta wenzake watano.

Ikumbukwe kumi na watatu hao wamefariki na wengine kujeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kukanyaga bomu la kutegwa ardhini kwenye eneo la Arabia, Kaunti ya Mandera.

Idara ya polisi imesema, kisa hicho kimetokea leo asubuhi na kwamba waliojeruhiwa wanaendelea kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mandera.

Tukio hili linajiri siku kadhaa baada ya baadhi ya mabalozi wa mataifa ya ughaibuni humu nchini kuwatahadharisha raia wake kuhusu tukio la kigaidi.


UGAID;MSHUKIWA;MANDERA