Chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kimemtetea vikali Katibu Mkuu wake Junet Mohammed dhidi ya madai kwamba alichangia kutokuwapo kwa maajenti katika baadhi ya vituo vya kupigia kura katika uchaguzi mkuu.
Katika taarifa ya msemaji wa kampeni za Raila Odinga, Prof Makau Mutua, Junet hakuhusika kwa njia yoyote na fedha zilizofaa kuwalipa maajenti inavyodaiwa.
Kadhalika, amemtetea Afisa Mkuu Mtendaji wa Kamati ya Kampeni Elizabeth Meyo kufuatia madai yayo hayo.
Amesisitiza viongozi wote wakuu katika chama walijizatiti kufanikisha majukumu yao katika mazingira ambayo ameyataja kuwa magumu.
Prof. Mutua ameongeza kwamba jukumu la kuzilinda kura ni la Tume ya Uchaguzi, IEBC wala si maajenti hivyo hawapaswi kulaumiwa.Kwa mujibu wa Mutua, katiba imeweka wazi kwamba IEBC inastahili kuendesha uchaguzi huru na wa haki, maajenti wakifanya tu kazi za uangalizi.