Naibu wa Rais, William Ruto ameitaka mahakama kuitupilia mbali kesi inayolenga kumzuia kuwania urais wakati wa uchaguzi mkuu ujao. Kesi hiyo imewasilishwa na Mkenya, Michael Kurungia anayesema kwamba Ruto ametekeleza majukumu yake ya Naibu wa Rais huku akitumia raslimali za serikali kuendeleza kampeni zake za kisiasa.

Katika kesi hiyo iliyowasilishwa mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Anthony Mrima, Kurungia aidha amelalamikia hatua ya Ruto kuendelea kutumia makazi yake rasmi mtaani Karen kwa mikutano ya kisiasa. Hata hivyo, Ruto kupitia kwa wakili wake, Elias Mutuma  amesema kwamba tangu achaguliwe pamoja na Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2017 hajawahi kukosa kutekeleza majukumu aliyopewa na Rais.

Ruto amesisitiza kwamba muhula wake wa kuhudumu utakamilika tu baada ya uchaguzi mkuu kufanyika ama iwapo atabanduliwa ofisini kupitia mswada wa kutokuwa na imani naye.

Aidha amesema kwamba malalamishi yaliyoibuliwa dhidi yake hayakustahili kuwasilishwa mahakamani ila kwa jopo la kusuluhisha mizozo ya vyama vya kisiasa. 


Ruto