Na, Beatrice Maganga Mabalozi wahimiza kuandaliwa kwa uchaguzi wa amani Mabalozi wa mataifa ya kigeni wanaohudumu humu nchini wametoa wito wa kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu huru na wa haki humu nchini. Wajumbe hao wametoa wito huo wakati walipofanya kikao na Kaimu Waziri wa Masuala ya Ndani ya nchi, Fred Matiang'i. Akiwahutubia wanahabari baada ya kikao hicho, Matiang'i amesema miongoni mwa yaliojadiliwa katika kikao hicho ni kuhusu namna maafisa wa usalama wanashirikiana na Tume ya Uchaguzi, IEBC ili kufanikisha uchaguzi mkuu huru na wa haki. Matiang'i amesema ni jukumu la IEBC kuandaa uchaguzi huku maafisa wa usalama wakihusishwa katika kuipa usaidizi IEBC kutekeleza jukumu lake la kikatiba. Wajumbe hao wametoa wito kwa serikali kuipa tume hiyo raslimali za kutosha ili kufanikisha maandalizi ya uchaguzi. Kikao hicho kimejiri wakati ambapo baadhi ya mataifa yametoa ilani kwa raia wake wanaoishi humu nchini kuwa waangalifu wakati huu wa uchaguzi. Mataifa ya Uingereza na Urusi ni miongoni mwa yale ambayo tayari yametoa ilani kwa raia wake.