Na Mike Nyagwoka

NAIROBI, KENYA, MVUTANO unatarajiwa kwenye mazungumzo ya kutaua utata wa IEBC baada ya kamati ya sheria bungeni kusisitiza kuwa itatoa ripoti yake chini ya kipindi cha wiki mbili zijazo licha ya juhudi zinazoendelezwa na kamati nyingine maalum.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Samuel Chepkonga amesema vikao vya mwisho kujadili mswada uliowaslishwa bungeni na mkenya Brian Nyikuri vitaandaliwa wiki ijayo kisha ripoti kuwasilishwa wiki moja baadaye.

Ikumbukwe kamati ya pamoja yenye watu 14 vilevile inajadili suala lilo hilo na inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake chini ya kipindi cha wiki nne zijazo. Kwa mujibu wa mkinzano huu kuna uwezekano wa bunge kupokea ripoti mbili zenye mapendekezo tofauti na hivyo kuathiri zaidi juhudi za kutatua utata ulioko.

Tayari mmoja wa wanachama wa kamati maalum ya watu 14 Dkt Bonny Khalwale amesema uamuzi wao ndio utakaokuwa na nguvu zaidi huku akiilaumu kamati inayoongozwa na Chepkonga kwa kujaribu kuhujumu utendakazi wa kamati yake.