Ndugu yangu Nelson Marwa amekuwa mwiba kwa wapwani tangu kuteuliwe kuwa kamishna wa kaunti ya Mombasa.

Na nikimnukuu Aden Duale kwa msemo wake kwa wakenya kuwa “pesa si ya mama yako’’, ningependa vile vile kumkumbusha Marwa kuwa Kenya sio ya “mama yako” ni ya wakenya wote.

 Ndugu Marwa ni mtu wa maajabu. Historia yake inaonyesha wazi kuwa yeye ni mtu anayeishi maisha ya kisiri na anayependa kujitenga na watu wengine. Ni vigumu kujua maisha yake — wengi hawajui bibi au watoto wake. Ni mtu msiri mno. Anadaiwa kukataa ulinzi na hata lile jumba alilopewa na serikali kwa madai ya kuhofia maisha yake. Kuna madai kuwa alikataa kulindwa na afisa wa polisi mwenye asili ya kisomali kwa kuwa hofu ya kushambuliwa na afisa huyo. Haya ni madai ninayopewa na wandani wangu katika afisi yake ingawa hatuwezi bainisha.

Marwa, mara kwa mara ameonekana kama kibaraka wa Jubilee, na wala sio afisa chapa kazi anayetaka kuwahudumia wakenya. Na kila mara anapofungua kinywa chake, kuu limekuwa kukashifu mambo asiyokuwa na ushahidi kwayo. Utamskia akiwatishia raia wapenda amani kwa mtutu wa bunduki kama alivyonakiliwa miaka ya nyuma akisema kuwa polisi wawaue kwa kuwapiga risasi  yeyote atakayepatikana na bunduki au kuwa mshukiwa wa kundi lolote haramu.

Katika uchaguzi mdogo wa Malindi Nelson Marwa amewaonyesha wakenya sura yake aliyokuwa akiificha kwa miaka na mikaka. Marwa alijaribu kugeuza malindi kuwa Uganda ndogo kwa kutumia maafisa wake wa polisi pamoja na wanajeshi walioonekana kupiga kambi Malindi kwa kuwashika kiholela wafuasi wa upinzani na hata kuwafungia kilifi badala ya Malindi.

Hofu yangu ni kwamba ndugu Marwa anatumiwa kama daraja la kuvuruga haki ya wapwani kwa kuwa ngome ya upinzani. Na sasa tayari ameanza alfu lela ulela ya kuwepo kwa kikundi cha MRC na vikundi vingine haramu. Wakenya wanafahamu fika kuwa  tangu kuapishwa kwa Uhuru Kenyatta kama rais, suala la MRC lilitokomea katika kaburi la sahau.

Mabadiliko ya hivi majuzi katika idara ya polisi pia ni ya kutia shauku kwani idadi ya maafisa wakuu waliopelekwa pwani ya Kenya wana husishwa na dhulma za tangu na jadi. Huenda uhamisho huu ukawa kama mojawapo ya njia ya serikali kujiandaa kulemaza kura za upinzani pwani ya Kenya. Sio pwani tu bali maeneo kama ya Kaskazini Kusini, Nyanza na Magharibi mwa Kenya mchezo huu umeanza kupangwa kimya kimya.

Duru zinaniarifu kuwa Robert Kitur rafikiye Marwa huenda akahamishwa hadi Nairobi kuafikisha malengo ya uchaguzi mkuu ujao katka mji wa Nairobi na viunga vyake.

Sisemi ndugu Marwa ni muovu, la, nasema kwamba kama mtumishi wa umma, na afisa mkuu wa polisi, anafaa kujiepusha na siasa chafu.

 Kwa maafisa wakabila, na hata wale wafisadi, ninawakumbusha kuwa Kenya ni kubwa kushinda miungu yenu midogo na senti zenu. Wawasihi msiingilie siasa na kubaka haki ya msingi ya wakenya mwaka wa 2017. Nawasihi mheshimu maamuzi ya wakenya. Nawasihi mjiepushe kuchoma taifa hili kwa shilingi mbili mnazopewa kuwadhulumu wakenya na sauti zao. Komeni kuwapigia wakenya kura bila maamuzi yao, komeni kuzua propaganda za kuwahofisha wakenya ili wasiweze piga kura.

Siandiki haya kuunga mkono chama fulani, bali naandika kuwataka mjue kuwa wakenya si wajinga, wakenya wamekomaa na wanafahamu hadithi zenu za longo longo na daganya toto jinga.

Safari hii hamna watoto wa kudanganya.  Hii ni Kenya mpya na wakenya wanaamini watashinda hata serikali ikijaribu kuiga tabia za Uganda na kutaka kutawala kwa nguvu. Wakenya bado hawajapata ukombozi wanayotaka na kukamia kila kukicha.

Ushindi wa mwaka wa 2017 utakuwa ushindi wa Eurobond, NYS, Chicken Gate, SGR na ukombozi wa pili tangu mwaka wa 1963. Huu utakuwa ushindi wa wakenya dhidi ya wezi wachache walio madarakani na wanaotaka kutawala Kenya kwa mabavu. Ushindi wa wakenya dhidi ya idara za ki-usalama zinazowadhulumu wakenya na zilizojaa ukabila, ushindi dhidi ya magaidi waliovalia suti na wanaofyonza damu ya wanyonge kila kukicha. Ashakum si matusi na kama nimekuudhi nasema pole. Mungu ibariki Kenya.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: mali@standardmedia.co.ke, FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Twitter: @mohajichopevu


moha jicho pevu;Mohammed Ali;Jicho Pevu