Mwaniaji urais wa Chama cha UDA, William Ruto ameahidi kumjumuisha kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka katika serikali yake endapo atashinda uchaguzi mkuu wa tarehe 9 mwezi ujao. Akizungumza wakati wa kampeni za Muungano wa Kenya Kwanza katika Kaunti ya Makueni, Ruto amemshtumu mshindani wake mkuu wa kisiasa, Raila Odinga kwa kumhangaisha Kalonzo kiasi cha kusitisha azma yake ya kuwania urais na kumuunga mkono kwa mara ya tatu.

Ruto aidha amemtaja Raila kuwa msumbufu na aliyezihangaisha serikali zilizopita japo anasema hilo litafikia kikomo mwaka huu.

Mgombea mwenza wa Ruto, Rigathi Gachagua kwa upande wake ameelekeza kampeni zake kwenye Kaunti ya Murang'a siku moja baada ya kushiriki mjadala wa wagombea wenza wa urais huku akiahidi kwamba endapo watatwaa uongozi wa nchi, suala la sare za maafisa wa polisi ambazo zilibadilishwa rangi pia wataliangazia katika baadhi ya marekebisho kwenye idara hiyo yatakayoangazia mishahara ya maafisa hao.

Kiongozi wa Chama cha ANC, Musalia Mudavadi ambaye pia ni mmoja wa vinara wa Kenya Kwanza ameendeleza mjadala kuhusu Raila kuwa mradi wa serikali sawa na mgombea ugavana wa Nairobi, Polycarp  Igathe. Mudavadi alikuwa akizungumza katika eneo la Dagoreti, jijini Nairobi wakati wa kampeni za kisiasa.