Kwa kipindi cha majuma mawili, macho ya Wakenya yataelekezwa katika Mahakama ya Juu ambapo kesi ya kupinga ushindi wa William Ruto katika uchaguzi wa urais Agostsi 9 inatarajiwa kuwasilishwa Jumatatu.
Chama cha Azimio, kinatarajiwa kuwasilisha rufaa hiyo kufikia saa nane mchana kabla ya kukamilika kwa makataa ya siku saba kisheria tangu Ruto alipotangazwa kuwa mshindi.
Jopo la Majaji saba likiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome, Njoki Ndung'u, William Ouko, Smokin Wanjala, Isaac Lenaola, Mohamed Ibrahim na Philomena Mwilu linatarajiwa kusikiliza na kuamua rufaa hiyo chini ya kipindi cha majuma mawili na kutoa mwelekeo wa kudumisha ama kubatilisha ushindi wa Ruto.
Hata hivyo, vikao kamili vinatarajiwa kuanza baada ya pande zote kuwasilisha nakala za utetezi wao mahakamani shughuli ambayo inatarajiwa kufanyika wiki hii.
Iwapo ushindi wa Ruto utadumishwa na mahakama, basi ataapishwa chini ya wiki moja na endapo utabatilishwa basi uchaguzi mwingine wa urais utafanywa ndani ya siku 60.
Mrengo wa Azimio ukiongozwa na Raila Odinga na Mgombea mwenza wake Martha Karua umeendelea kusisitiza kuwa taifa litakuwa na amani endapo tu haki itatendeka.
Upande wa Kenya Kwanza nao ukiongozwa na Ruto umekariri kwamba uko tayari kutetea ushindi wake.