Na Beatrice Maganga

Rais Uhuru Kenyatta amelazimika kukatiza safari yake hadi nchini Angola kufuatia shambulio linaloaminika kutekelezwa na wanamgambo wa Al Shabaab kwenye Kaunti ya Mandera. Rais alitarajiwa kusafiri kesho hadi Luanda Angola kulihudhuria kongamano la usalama. Naibu wake, William Ruto atalazimika kusafiri kuhudhuria mkutano nchini humo kwa niaba ya Rais. Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Msemaji wa Ikulu Manoah Esipisu amesema Rais amechukua hatua hiyo, ishara ya kuomboleza na familia zilizofiwa kutokana na uvamizi huo. Aidha Rais amewashauri wananchi kushirikiana na maafisa wa usalama kulilinda taifa dhidi ya magaidi. Hayo yakijiri, Magavana saba wa eneo la Kaskazini Mashariki ya nchini wamelishtumu vikali shambulio lililotekelezwa mjini Mandera usiku wa kuamkia leo ambapo watu kumi na wawili waliuliwa na wengine kujeruhiwa. Viongozi hao wamelalamikia kuendelea kudorora kwa usalama licha ya kuwapo kwa maafisa wa usalama. Gavana wa Mandera Ali Roba ameeleza kusikitishwa na shambulio hilo linaloaminika kutekelezwa na wanamgambo wa Al Shabaab akisema lengo kuu si kuzua tofauti za kidini bali kusambaratisha uchumi wa kaunti hiyo.Aidha ameshangazwa na kudorora kwa usalama ilhali kuna maafisa wa usalama kwenye kaunti hiyo. Gavana wa Lamu Issa Timamy kwa upande wake ameitaka serikali kuimarisha mbinu zake za kudumisha usalama ikizingatiwa kuwa kaunti zote za Kaskazini Mashariki ya nchini zimekuwa zikilengwa mara kwa mara na magaidi. Naye Gavana Nathif Jama wa Garissa ameisihi serikali kuwakamata mara moja wahusika wa mauaji hayo yaliyotekelezwa katika Hoteli ya Bishaare usiku wa kuamkia Jumanne. Imebainika kuwa vilipuzi vya kujitengenezea vilitumika wakati wa shambulio hilo ambalo limejiri siku chache tu baada ya baadhi ya viongozi wa Kaskazini Mashariki ya Nchi kulalamikia mwendo wa kobe wa ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wa Kenya na Somalia. Imebainika kuwa licha ya serikali kuanza ujenzi wa ukuta huo miezi kumi na minane iliyopita, kufikia sasa ni milingoti tu iliyowekwa katika eneo la umbali wa kilomita 1.8 pekee. Ikumbukwe serikali ilisema itajenga ukuta wa umbali wa kilomita 360 ikiwa ni njia mojawapo ya kuwazuia magaidi kujipenyeza nchini.  

 


William Ruto;Uhuru Kenyatta;Mandera;Garissa