Na,Sophia Chinyezi Mwanaharakati Okiya Omtata amewasilisha kesi mahakamani kupinga sheria ya viwango vipya vya riba iliyoidhinishwa na Rais Uhuru Kenyatta. Sheria hiyo inazizuia benki kutotoza riba ya zaidi ya asilimia 14.5 kwenye mikopo inayotolewa na benki. Omtata anasema riba hiyo ingali juu na inakiuka katiba. Aidha anasema benki zimekosea kwa kuweka viwango vya riba kwa kuzingatia iliyowekwa na Benki Kuu Nchini, badala ya zile zinazotolewa na Mwongozo kuhusu Riba KBRR. Kadhalika amesema tofauti kati ya riba iliyoratibiwa kwenye sheria na kile kinachotozwa na benki ni asilimia 1.6. Kwenye hoja aliyoiwasilisha katika Mahakama ya Milimani, Omtata anaitaka mahakama kuhakikisha Benki Kuu na Shirika la Benki Nchini KBA zinazingatia viwango vya riba vinayotolewa na KBRR na si Benki Kuu. Baadhi ya benki nchini zimepunguza viwango vya riba kwa wateja waliochukua mikopo awali na wa sasa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini mswada wa marekebisho wa benki wa mwaka 2015.