Kamati ya Kushughulikia Mizozo ya Tume ya Uchaguzi, IEBC imetupilia mbalimbali kesi iliyowasilishwa mbele yake na kiongozi wa Chama cha Third Way Alliance, Ekuru Aukot ya kutaka Raila Odinga azuiwe kuwania urais.

Kamati hiyo imesema kwamba Raila aliteuliwa kwa njia halali kuwania urais kupitia Chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kinyume na madai ya Aukot kwamba Raila aliidhinishwa bila kuwa mwanachama wa chama chochote cha kisiasa.

Kamati hiyo hata hivyo imesema haina mamlaka ya kufanya uamuzi kuhusu madai yaliyoibuliwa na Aukot kwamba uteuzi wa Raila unafadhiliwa na serikali vile kwamba anatumia raslimali za serikali kuendesha kampeni zake.

Raila aliwakilishwa na mawakili mbalimbali akiwamo Velma Maumo katika kuwasilisha utetezi wake mbele ya kamati hiyo ambao walisisitiza kwamba aliteuliwa kuwania urais kupitia Azimio kwa kuzingatia sheria.

Wakati uo huo, Mgombea wa Urais wa Chama cha Safina Jimi Wanjigi amepata pigo jingine baada ya kamati hiyo ya IEBC ya kusuluhisha mizozo kukataa kesi aliyoiwasilisha kuitaka kumuhoji mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo George Mburu alisema hawana mamlaka ya kumhoji mkubwa wao kufuatia uamuzi wake wa kutomuidhinisha Wanjigi kuwania urais.

Kamati hiyo leo hii inatarajiwa kuendelea kutoa maamuzi kuhusu malalamishi yaliyowasilishwa na wawaniaji wengine wa urais wakiwamo,  Walter  Mong'are maarufu Nyambane vilevile Reuben Kigame.