Mahakama ya Juu imesikiza kesi ya kupinga kuharamishwa kwa mpango wa BBI kwa siku ya pili leo hii, ambapo majaji wamewakabili mawakili wa serikali kwa maswali mazito kuhusu hoja zao za kutetea BBI.

Aidha, mawakili wa upande unaopinga BBI wamewasilisha hoja za kukosoa mchakato wa BBI na kukariri kwamba katiba ya Kenya ina vifungu ambavyo haviwezi kubadilishwa kiholela.

Majaji wa mahakama hiyo waliibua masuala tata kuhusu hoja za mawakili wa upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Paul Kihara wakitaka ufafanuzi zaidi.

Jaji Mkuu Martha Koome na Jaji William Ouko walitaka kuelezwa ni kwa nini Rais alianzisha BBI, kisha baadaye kuteua kamati ya kuendeleza mpango huo, iwapo alikuwa na haki ya kuasisi mchakato wa kuifanyia katiba marekebisho.

Mawakili  George Oraro na Paul Kimani wamemtetea Rais wakisema alikuwa tu mwanzilishi wa mpango huo wala si mwasisi wa mswada wa BBI.

Kuhusu suala tata la muundo wa kimsingi wa katiba, basic structure doctrine, Jaji Smokin Wanjala alitaka ufafanuzi wa ni kwa nini mfumo huo haufai kutumika nchini Kenya.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Prof. Githu Muigai amesema mfumo huo haufai kutumika Kenya kwa sababu hautambuliki kisheria.

Aidha, suala la kinga ya rais kikatiba, liliangaziwa kwa kina na Mwanaharakati Isaac Aluochier ambaye amesema hakuna kinga kamilifu kwa rais katika katiba, na kwamba anaweza kufunguliwa mashtaka ya masuala ya kisheria na uchaguzi wa urais.

Kauli sawa na hiyo imetolewa na Nelson Havi, wakili wa Mwanauchumi David Ndii na Mwanahakati Jerotich Seii.

Rais Kenyatta kupitia Wakili Waweru Gatonye, ??amekariri kwamba mahakama za chini zilikiuka sheria kwa kusema anaweza kushtakiwa.

Vikao vya kusikiza kesi hiyo vitakamilika Alhamisi.