Mtihani ya KCSE umeingia wiki ya pili huku serikali ikiendeleza msako mkali dhidi ya wanaodaiwa kuhusika na udanganyifu wa mitihani hiyo.
Kufikia Ijumaa, washukiwa zaidi ya 7 walikuwa wamekamatwa kwa kuchangia katika udanganyifu huo kwenye Kaunti ya Kericho.
3 miongoni mwao walikuwa walimu wawili wa somo la Kemia na mhudumu wa maabara ambao waliwasaidia maafisa wa upelelezi kuwatambua wenzao kabla ya kufikishwa mahakamani.
Kinaya ni kwamba Waziri wa Elimu Profesa George Magoha amekuwa akijipiga kifua kila mara akisisitiza kwamba kusingekuwa na udangayifu wakati wa mtihani wowote.
Kando na udanganyifu, waliokamatwa walipatikana na mitihani ya karatasi za Kemia za mwaka huu zikiwa kwenye simu zao hata kabla ya mtihani wenyewe kufanyika.
Tukio hili linadhihirisha wazi uozo katika Baraza la Kitaifa la Mitihani KNEC ambalo sharti vilevile liwajibishwe na kujibu maswali kadhaa kama vile; ni vipi yaliyomo kwenye karatasi hizo yanapenyeza na kuwafikia walimu hadi mashinani?
Na je, ni wangapi waliozipata karatasi hizo na ambao pengine hawajakamatwa?
Iwapo mitihani ya KCPE na KCSE inachapishwa Uingereza, nani anayefanikisha udangayifu huu? Ni kisa cha kikulacho ki-nguoni mwako?