Knec imeorodhesha mikakati kemkem ya kudhibiti wizi wa mitihani ya kitaifa ili kulirejeshea baraza hilo hadhi inayostahili  Picha:Hisani

Anasema mwimbaji maarufu kutoka nchini Tanzania, Mrisho Mpoto, kuwa ukikanyagwa maksudi kwenye sherehe ya harusi huambiwi pole, lakini kwenye tafrija za matanga huambiwa samahani!

Kauli hiyo hapo juu yaendana sambamba na jinsi hali ilivyokuwa nchini Kenya mwaka jana, punde tu baada ya kutangazwa matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la nane, KCPE, sawia na matokeo ya mtihani wa taifa kidato cha nne, KCSE.

Matokeo hayo yaliandamwa na furaha kwa washindi, sherehe ya harusi, na vilio kwa baadhi, tafrija za matangani. Leo hii basi tuandame tafrija za matangani maana wiki hii Baraza kuu la Mitihani nchini, KNEC, limenena, limesema na ni kama limeanza kunguruma. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa maalum kuhusu mitihani ya taifa mwaka huu iliyochapishwa mnamo Jumatatu wiki hii katika gazeti letu la Standard.

Tutachokonoa taarifa hiyo baadaye kuihusu mikakati ya KNEC kuzima na kuzika kabisa visa vya wizi wa mitihani kwenye kaburi la sahau.

Lakini kwa sasa hebu turejeshane nyuma na kukunana vichwa japo kiduchu. Itakumbukwa kuwa mitihani ya KCPE na KCSE mwaka jana ilikumbwa na visa si haba vya wizi. Mitandao ya jamii ilishamiri maswali ya mitihani hiyo hivi kwamba baadhi ya wadau walikuwa wakiomba mitihani hiyo kufutuliwa mbali. Lakini wepi! Sikio la kufa jamani.

Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kabisa mwaka huu. Punde baada ya waziri mpya wa elimu Dr. Fred Matiang’i kuchukua nafasi ya mtangulizi wake Profesa Jacob Kaimenyi, tufani sasa laonekena katika wizara ya elimu hususan KNEC. Sio tu kwamba Dr. Matiang’i alilivunjilia mbali baraza la KNEC, lakini zilikuwa habari zilizopokelewa kwa hisia mseto pale mameneja wakuu wanane wa baraza hilo wakiongozwa na Afisa Mkuu Mtendaji Bw. Joseph Kivilu, waliposimamishwa kazi na kufunguliwa mashtaka!

Baraza hilo likapata nguvu na uhai mpya, likabuniwa upya chini ya uongozi wa aliyekuwa naibu mkuu wa chuo kikuu cha Nairobi Profesa George Magoha. Na sasa cheche za utenda-kazi katika baraza hilo zimeanza kuonekana.

Ki vipi?

Ndio hapo basi kurejelea taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti letu la The Standard hapo Jumatatu na kuorodhesha mikakati kemkem ya kudhibiti wizi wa mitihani ya taifa ya mwaka huu, ili kulirejeshea baraza hilo hadhi inayostahili.

Mbali na kuwa na watungaji wapya wa mitihani (labda), baraza hilo linalenga wafanyikazi wake kuzingatia kiapo cha usiri, na hata ikibidi kuandaa upya mitihani ya taifa. Aidha, vigezo na masharti mapya vitawaandama wasahihishaji wa mitihani hiyo, miongoni mwa mikakati chungu nzima ya kuzuia wizi wa mitihani.

Ripoti iliyochapishwa siku si nyingi zilizopita ilifichua kuwa njama za wizi wa mitihani zimekuwa zikiwahusisha wana Tume ya Huduma za Walimu, TSC, walinzi wa mitihani, walimu na wanafunzi hasa wa vyuo vikuu. Ama kweli kulikuwa na uozo wa fondogoo kwenye KNEC. Watahiniwa wetu – hasa waliosajiliwa mwaka huu – walimu, wazazi na wadau wa elimu wanasubiri kwa hamu na hamumu. Je, magego mapya yenye kung’ata ya KNEC mpya chini ya Profesa George Magoha yatakata kabisa shina na mzizi wa wizi wa mitihani na kuwapa Wakenya tabasamu na imani, ama kitasalia kisa cha kuchimba shimo na kuziba tundu?

Mwandishi wa makala haya ni mhariri wa habari za michezo @radiomaisha, mbali na kuandaa na kupeperusha hewani kipindi maarufu cha lugha ya Kiswahili nchini NURU YA LUGHA kila Jumamosi kuanzia saa moja asubuhi. Wasiliana naye kwa barua meme: alikauleni@gmail.com, akaulen2@standardmedia.co.ke, twitter: @alikauleni, FB: alikauleni or Hassan mwana wa Ali.