Je, ni nani anayesema ukweli hapa? Je, ni nani wa kusingiziwa hapa? Je, ni yupi aliyetoa ahadi za uongo jukwaani? Haya ni baadhi ya maswali ambayo Wakenya wengi wanazidi kujiuliza.

Hatua aliyoichukuwa kiongozi wa walio wengi bungeni Aden Duale kudinda kutoa orodha ya wafadhili wa ugaidi ni pigo kuu kwa waliopoteza wapendwa wao katika mashambulizi ya kigaidi. Tukio hili limewaacha wengi vinywa wazi baada ya Duale kubadili msimamo wake wa awali.

Jambo hilo ni kejeli kubwa kwa Wakenya hasa waliowapoteza jamaa zao katika shambulizi la kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa ambako wanafunzi wapatao 148 walifariki. Inastaajabisha mno kwani serikali yetu haijachukulia suala hilo hatua inayostahili.

Serikali yafaa ifahamu kuwa ufanisi wake katika sekta ya usalama utapimwa kulingana na kiwango cha hali ya maisha ya Wakenya na si idadi ya miradi ambayo imezinduliwa. Wakenya wanatathmini ishara ya ufanisi katika hali ya maisha yao na sio uwingi wa miradi.