Wazee Wasuba katika mojawapo ya ngoma zao asilia. Jamii ya Suba inafurahia kuwasilishwa bungeni na mmoja wao Mbunge John Mbadi.

Kuna makabila mengine ya zamani ambayo yamebakia na watu wachache tu wanaofahamu asili mila na desturi za wavyele wao. Hii ni kutokana na uhamaji na kumezwa na makabila mengine. Wasuba ama Abasuba  ni moja ya makabila ya watu wa Kenya ambao wanaongea lugha ya Kisuba lakini wengi wao huongea  Kijaluo. Jina Suba huwakilisha makundi matatu tofauti ya watu  wanaoishi Kusini Magharibi mwa Kenya katika eneo la Nyanza Kusini na mamkundi hayo ni Suba (Abasuba) Irenyi (abirienyi ) na Kunta (Abakunta). Kundi la Suba liliingia Kenya kutoka eneo la Mara Tanzania. Ingawa Wasuba huchukuliwa kama kabila, wao ni kabila dogo tu lililokuwa chini ya kabila kubwa la Wagirango lililojumuisha makabila mengine madogo kama vile Wategi na Wagire.

Kwa hiyo basi wao hujulikana pia kama Wasuba-Girango au Wasuna-Girango. Wasuba wanaishi viungani vya mji wa Migori na lugha yao asilia ni Kisuba iliyokaribiana maeneo yanayojulikana na lugha ya Kikuria. Walihamia Afrika Mashariki  wakitokea Misri kaskazini mwa Afrika. Girango ndiye mvyele  wa Wasuba halisi.  Mtegi ni mototo wa Girango, na alitoka Kitgum,Uganda na akatembea mpaka Karachuonyo. Na hapo walikaa kwa muda mrefu na wakahama mpaka nchi ya Wakipsigis.    Ongombe akahamia huko Kamagambo, ambapo hata hivi sasa bado wengi wao wanaishi huko na wanajulikana kama Wategi, ukoo wa Kamagambo au Kanyingombe.    

Kuna kabila la watu nchini Tanzania, mkoani Mara wanaojiita Wasuba.  Watu hawa haswa hujulikana kwa pamoja kama Wasuba-Simbiti. Wasweta katika kundi hili la Wasuba-Simbiti ndio hupatikana hata nchini Kenya,na ni Waluhya (Maragoli) . Walitoka sehemu ya Masaba Uganda.

Safari yao hiyo iliwafikisha sehemu ya Umaragoli  Vihiga. Wasuba walimezwa na majirani na lugha yao ya Kisuba pamoja na mila zao kutokomea kabisa. Kwa sasa Wasuba-Girango wote huongea  Dholuo…   Idadi yao nchini Kenya inakadiriwa kuwa 200,000 na wao ndio wakazi wa wilaya ndogo za Suba Mashariki na Suba Magharibi katika sehemu ya Migori. Kumezwa kwa kabila la Wasuba na Wajaluo kulitokana na kuoana kwani tokea ujio wa Wajaluo, watu hawa ni majirani. Isitoshe, kabila la Wajaluo wa Kenya na Tanzania si Waniloti halisi, bali ni mchanganyiko wa Wabantu na Waniloti. Wao ni mkusanyiko wa Wajaluo waliotawanyika kutoka kwa makundi mbalimbali ya Waluo ndiyo maana hawana jina maalum la kujitabulisha kama vile makabila ya Wajaluo wa Uganda na Sudan. Mkusanyiko huu ulichanganya damu na mila na Wabantu kutokana na uhamiaji na ufugaji. 

Baadhi ya jamii ya Wajaluo wanaoaminika kwamba walikuwa Wabantu na walibadilika kuwa  kwa namna sawa na ile ya Wasuba ni Wakasgunga,Wakamagambo, na wengineo.  Wasuba wengi hujitambulisha kama Waluo kwani wameathiriwa na kuridhia mila na desturi za Kiluo. Katika jamii ya Wajaluo, wao huwekwa kwenye kikundi kinachojulikana kama Joka Jok pamoja na Kamagambo, Kasgunga, Konyango Rabala, Muksero, Kanyamkago, Nyakach, Kisumo, na Kano.

Itikadi za Wasuba kadhaa zinafanana na za Wakuria. Walikuwa na bado wanathamini mpaka sasa mila za tohara, kutia watoto jandoni, hususan watoto wa kiume.  Hata kama Wasuba waliathirika kimila, bado wanathamini majina yao   ya kijadi, na majina hayo kwa kiasi hufanana na majina ya Wakuria. Kwa mfano Chacha, Marwa, Matiku, Mbusiro, Matinde, na Mwabe.