Kesi ya kubaini mauaji ya Farida Kadzo, mwanafunzi wa kidato cha pili inatarajiwa kurejea mahakamani hii leo.
Hii ni baada ya Jaji Wendy Muchemi kuhairisha kesi hio hapo jana baada ya mashahidi wawili kuto kauli yao kulingana na mauaji hayo.
Kazdo, ambaye alikuwa na umri wa miaka 17, aliuawa kwa kudungwa kisu Juni, 6 mita chache kutoka nyumbani kwao kwenye eneo la Mferejini, Kijipwa katika Kaunti ya Kilifi, mwendo wa saa mbili usiku na kufariki dakika chache baadaye.
Rose Umazi, shahidi katika kesi hio alisema kwamba mwili wa mwenda zake ulikuwa na majeraha kadhaa sehemu tofauti mwilini ikiwemo shingo yenyewe.
Kulingana na kauli yake, marehemu alikuwa na majeraha kadhaa ikiwemo ya kukatwa sehemu ya koo kabla kisu kudungwa upande wa kulia wa juu wa shingo na kuchomoza upande wa kushoto.
Umazi aliambia mahakama kuwa, mbali na majeraha hayo ya shingo, Kadzo pia alikuwa na majeraha upande wa kulia wa bega na viganjani.
Shahidi huyo ambaye ni shangazi wa marehemu aliweza kukitambua kisu alichochomwa nacho ambacho kilikuwa na damu iliyokauka kilichowasilishwa mbele ya mahakama na upande wa mashtaka.
Kwa mujibu wa kauli yake, kisu hicho dicho kilikuwa kikitumiwa na mshukiwa mkuu Lewis Kazungu, 22, amaye inasemekana alikuwa mpenzi we marehemu.
Umazi alisema kuwa Kazungu alikuwa akikitumia kisu hicho katika shughuli zake za kugema pombe ya mnazi, kazi ambayo alikuwa ameifanya kwa muda wa miezi sita baada ya kuajiriwa na mama wa marehemu.
Umazi amekumbuka matukio ya kabla Umazi kufariki, akianza na jinsi wawili hao walivyokutana pembezoni mwa boma la kina Kadzo na kuzungumza kabla ya kurejea kwa chakula cha jioni.
Baadae mshukiwa, alitangulia kuondoka, kisha Kadzo akafuata.
Huku Kazungu akienda kwaeke, Kadzo inasemekana alienda kuchukua simu aliyokuwa ameipeleka kuchaji.
Muda mchache baadaye, Umazi alisikia sauti ya Kadzo akipiga mayowe kisha akanyamaza ghafla; kilichofuata walimuona akiwa ameanguka nje ya jiko, mwili ukiwa umeloa damu huku mkono ukiwa umetoa kisu shingoni.
Henry Randu, Naibu Chifu wa Kinani Makomboani, aliambia mahakama kuwa alipokea simu saa tisa alfajiri siku iliyofuatia ya tarehe saba kutoka kwa Safari Karisa Mitingi ambaye ni binamu wa mshukiwa.
Kulingana na Randu, bwana Mitingi alitaka ushauri kutoka kwake kwani Kazungu alikuwa amemuua mkewe kwa kumdunga kisu baada ya kutofautiana.
Randu alisema Mitingi alikiri kuwa baada ya mshukiwa kutekeleza kitendo hicho alitoweka asijulikane aliko, akimshauri ahakikishe amewasilisha ripoti polisi.
Baadae, mshukiwa alionekana shambani kwao kwenye eneo la Makomboani akiwa katika harakati za kutoka kujinyonga huku akiwa ni kama amechanganyikiwa.
Randu alifika kwenye eneo hilo na kumchukua, kisha akamwasilisha kwa polisi wa eneo hilo waliowasiliana na maafisa wa Kituo cha Kijipwa ambao walimchukua na kumzuilia.
Jaji Jaji Wendy Muchemi aliagiza kesi hiyo kuendelea kusikilizwa leo, upande wa mashtaka ukiratibiwa kuwasilisha shahidi mwingine mmoja.
Kesi hii inajiri huku Kenya leo ikiwa imeungana na mataifa mengine duniani kuanza maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati wa Kukomesha Unyanyasaji wa Kijinsia chini ya kaulimbiu, ‘Unganeni Kukomesha Unyanyasaji wa Kidijitali dhidi ya Wanawake na Wasichana Wote’.
Shirika la International Justice Mission linafuatilia kwa karibu kisa cha mauaji ya Kadzo, ambaye pia alikuwa mama wa mtoto mwenye umri wa miezi tisa, kuhakikisha anapata haki.