Serikali imeanzisha mikakati ya kudhibiti kilimo cha mahindi na bei ya unga wa ugali kufuatia kuchelewa kwa mvua ya kufanikisha upanzi wa mimea mwaka huu.

Akithibitisha kupokea malalamishi ya Wakenya wengi kuhusu ongezeko la bei ya unga wa mahindi, Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri amesema upungufu wa mahindi yanayoweza kukidhi hitaji la wananchi kutoka kwa wakulima wa humu nchini ndiyo sababu kuu inayoathiri bei ya unga.

Amesema Kenya ina uwezo wa kuzalisha magunia ya kilo tisini kati ya milioni 40 na 44 za mahindi ikilinganishwa na hitaji la Wakenya ambalo linafikia magunia milioni 50 kila mwaka. Amesema hali hiyo hudhibitiwa kwa soko huru baina ya Kenya na mataifa ya Afrika Mashariki na yale ya Kusini.

Kuhusu kuchelewa kwa mvua ya kufaulisha upanzi wa mwaka huu, Waziri Kiunjuri amesema utafiti wa idara ya utabiri wa anga umeonesha kuwa huenda kiwango cha mvua kikawa kidogo zaidi mwaka huu, hali ambayo itaathiri ukulima. Amewashauri Wakulima kuanza shughuli za upanzi mapema kuanzia tarehe 15 mwezi huu kwa kupanda mimea inayokuwa kwa haraka.

Mapema leo viongozi wa Kidini nchini wakiongozwa na Mwenyekiti wa baraza la maimamu katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa Abubakar Bini, walitoa wito kwa serikali ya kitaifa kubuni mikakati ya dharura ili kudhibiti ongezeko la bei ya unga wa mahindi.