Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia Mohamed Farmaajo ,wamefanya mazungumzo kuhusu mzozo wa kunadiwa kwa maeneo ya bahari yaliyo mkapani pa Kenya na Somalia. Mkutano huo umeongozwa na Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed hapa jijini  Nairobi.

Kwenye ujumbe wake katika mtandao wa kijamii wa twiter baada ya mazungumzo hayo, Abiy amesema mataifa haya mawili yameafikiana kushughulikia mzozo wa kidiplomasia .Ahmed Aby amesema wawili hao wanatarajiwa kuendeleza mazungumzo muhimu ili kukuza umoja wa kieneo ,amani,usalama  na  maendeleo. Juma lililopita Abiy, aliongoza mikutano miwili tofauti ya kidiplomasia na Kenyatta na Farmaajo.

Mwezi uliopita Kenya ilimtimua Balozi wa Somalia hapa nchini Mohamud Ahmed Nur, na kumwagiza Balozi wake nchini Somalia Generali mstaafu Lucas Tumbo  kurejea Kenya mara moja. Kenya imeilaumu Somalia  kwa kuuza maksudi sehemu yenye gesi na mafuta inayosemekana kumilikiwa na Kenya.

Kenya ilikuwa imepinga ombi la Somalia katika Mahakama ya Kimataifa ya  ICJ September 2016 kuhusu sehemu hiyo inayozozaniwa ikisema kwamba mahakama hiyo ilikosa uwezo wa kushughulikia mzozo huo huku ICJ ikipuuzilia mbali ombi la Kenya.

Mahakama hiyo baadaye ilitenga Tarehe 18 Juni 2018 kwa Somalia kuwasilisha mapendekezo yake huku Kenya ikitengewa Disemba 18, 2018 kutoa mapendekezo yake kuhusu mzozo huo.