Na Beatrice Maganga, Willy Khaemba

Polisi mjini Eldoret wamemtia mbaroni mwanamume mwenye umri wa miaka 36 anayedaiwa kumuua mpenziwe mwenye umri wa miaka 26 kwenye Mtaa wa Kapsoya. Mshukiwa wa mauaji ametambuliwa kuwa David Siloba.  Polisi wanasema mwili wa marehemu ulitumbukizwa katika tangi la maji huku ukiwa na  majeraha mabaya kichwani na vidole kukatwa.

Haron Kipyego, rafiki wa karibu wa mshukiwa wa mauaji hayo David Siloba, amesimulia kuhusu tukio hilo la mapema leo alipopigiwa simu na mshukiwa, aliyemweleza kuwa amemuua mkewe na kwamba alitaka kuuteketeza mwili.  Kipyego aidha aliamua kuripoti kwa polisi kuhusu tukio hilo licha ya mshukiwa kumtaka asifanye hivyo.

Kisa hicho aidha kimewaacha wakazi wa Kijiji cha Mariakani na mshangao huku baadhi wakielezea namna ndoa kati ya wawili hao ilivyokumbwa na utata. Wakazi aidha wanadai mshukiwa ni  mraibu wa dawa za kulevya, na kwamba mara kwa mara wawilli hao walionekana katika maeneo ya burudani

Kwa sasa maafisa wa polisi wanamzuilia mshukiwa, huku mwili wa mwendazake ukipekekwa katika Chumba cha kUhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Moi. Katika siku za hivi karibuni visa vya wapenzi kuuana vimekuwa vikiripotiwa kila kukicha.Siku chache zilizopita mwanamke mmoja mjamzito aliuliwa na mumewe kwenye Mtaa wa Kahawa Sukari, jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa majirani, walimsikia mwanamke huyo kwa jina Beryl Odhiambo akipiga mayowe kwa takriban saa nne kisa kunyamaza na badaye kubainika alikuwa ameuliwa na mumewe kwa jina Laiko Osuri ambaye kwa sasa anazuiliwa na polisi. Aidha kwenye kisa kingine, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Ufundi cha Kaboi kilicho kwenye Kaunti ya Nandi aliuliwa na mpenziwe kwa kudungwa kisu.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 21 alifumaniwa na mpenziwe akiwa katika chumba cha maankuli na kudungwa kisu mara kadhaa shingoni na kifuani. Ilidaiwa kwamba msichana huyo aliuliwa kwa kukatiza uhusiano na mpenziwe ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo hicho hali iliyomgadhabisha. Tukio hilo lilichangia kufungwa kwa chuo hicho huku uchunguzi ukiendelea.