Serikali imefungua akaunti ya kutuma michango ya kuwasaidia waathiriwa wa mkasa wa Solai kufuatia maji kupasua kingo za bwawa la Patel, Solai Nakuru. Unaweza kutuma fedha kupitia M-Pesa Paybill 10000, Account -Solai.

Hayo yanajiri huku familia za watu 37 miongoni mwa 48 walioaga dunia zimefanikiwa kutambua mili ya jamaa zao. Ripoti iliyotolewa na maafisa wanaoongoza shughuli hiyo ni kwamba watu arubaini na wanne wangali wanatafutwa.

Mapema leo, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DCI George Kinoti amesema tayari ameanza uchunguzi wa kubaini chanzo cha kuporomoka kwa kuta za Bwawa la Patel na kusababisha vifo hivyo.

Msemaji wa Serikali Eric Kiraithe amesema hali hiyo ingezuiwa iwapo kiwango cha maji kingepunguzwa, kwa vile yalikuwa yamejaa kupita kiasi kutokana na mvua kubwa. Kiraithe amesema huenda mmiliki wa bwawa hilo akachukuliwa hatua.

Hayo yakijiri, Umoja wa Ulaya umeahidi kutoa kwa waathiriwa wa mkasa huo.

Mapema leo, wakazi wa Solai walikimbilia usalama baada ya uvumi kuenea kuwa kingo za bwawa jingine linalomilikiwa na Manskul Patel, zimeporomoka. Hata hivyo wataalam walituliza hali hiyo na kuwahakikishia kuwa maji katika bwawa hilo yamepunguzwa ili kuzuia athari sawa na zilizoshuhudiwa.