Na CHINYEZI
Zikiwa zimesalia siku hamsini na sita kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8 kuandaliwa, Tume ya Uchaguzi IEBC na baadhi ya wabunge wameeleza wasiwasi kufuatia utayarifu wa uchaguzi huo, iwapo Mkenya yeyote atawasilisha kesi mahakamani kupinga hatua ya kuipa kampuni moja ya Dubai zabuni ya kuchapisha karatasi za uchaguzi.

Akizungumza alipofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki na Masuala ya sheria, AFisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Ezra Chiloba amesema wanafanya wawezalo kukamilisha matayarisho yake kabla muda kukamilika na kufanya maamuzi mazito kwa kuzingatia Sheria za Uchaguzi.  Kadhalika amesema wana imani watakamilisha kusikiliza kesi zilizotokana na uteuzi kufikia Jumanne wiki ijayo.

Kadhalika amesema iwapo kutatokea mtu atakayeipinga zabuni iliyotolewa kwa kampuni ya Al Ghurair na kuilazimu IEBC kuanza upya shughuli ya kutafuta kampuni nyingine ya kuchapisha karatasi za uchaguzi, hali hiyo huenda ikasababisha matatizo katika maandalizi ya uchaguzi.

Hayo yakijiri, IEBC imesema mikakati mwafaka imewekwa kuhakikisha vifaa vya teknolojia vilivyonunuliwa vinafanya kazi wakati wa uchaguzi mkuu. Kaimu Mkurugenzi wa Masuala ya Mawasiliano katika IEBC, Chris Msando amesema vifaa vya Mfumo wa Usimamizi wa Uchaguzi KIEMS, vilivyonunuliwa na IEBC vitafanya kazi vyema, kwa kuwa vimefanyiwa majaribio ya kutosha ili visifeli, ilivyoshuhudiwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2013.

Kufikia sasa tume hiyo ina vifa elfu thelathini na vitano vya KIEMS. Vifa elfu kumi na moja miongoni mwazo vilitumika katika shughuli ya ukaguzi wa sajili ya wapiga-kura.