Ufisadi watumaliza Picha: Hisani

Mnamo Jumanne wiki hii nikiwa mtaa wa Mwiki, eneo la Kasarani, nilishuhudia kisa ambacho kingali kunipiga moyo hadi sasa.

Nilikuwa nimekwenda eneo hilo kuwanasa wanafunzi na walimu wao kuhusu maandalizi ya mitihani ya taifa.
Aidha, nilitaka pia kujua ni kwa vipi walivyo na imani na timu mpya iliyochukua uongozi wa Baraza la Taifa la Mitihani Nchini kutokana na uozo wa wizi wa mitihani mwaka jana ulijitokeza katika afisi iliyokuwepo KNEC.

Sakata ya wizi wa mitihani mwaka jana ilituacha nchi nzima tukiwa hoi-bin taaban! Na hata jirani zetu kutusema pembeni: “Wakenya nyie ni wajanja wa mjini na majizi makubwa ati.

Kusema “mafisadi’ ni nafuu. Kheri tu tuseme nyinyi ni “mifisadi’”. Kauli hiyo kutoka kwa jirani sio kwamba tu inauma, lakini pia inakeketa maini.

Hata majirani zetu hao wametuopoga namna mtu aogopavyo joka la mdimu! Baada ya kufanya mahojiano yangu mtaani Mwiki, nililiona gari kweche la baraza la mji wa Nairobi likiwa limeegeshwa pembeni.

Ndani mlikuwa mmepakiwa akina mama wauza mboga. Wamepakiwa kama dagaa kikaongoni! Kila mmoja alikuwa ‘akinunua’ uhuru wake. Kisa na maana ni kuwa walikuwa wakifanya biashara ya kuuza mboga bila risiti ya jiji wa Nairobi!Iliniuma sana.

Picha hiyo ingali akilini mwangu. Nikuulize gavana wa jiji la Nairobi: “Hivi ushuru tulipao wendapi? Kwa nini maskini kumla maskini mwenzake? Mama muuza mboga huondoka mchana kutwa akienda nyumbani akiwa na shilingi mbili, leo hii weye waje kumpokonya shilingi hizo mbili.

Hadi lini jamani? Mbona hata mwahali pa kuuzia mboga ni mavumbi tupu. Hana choo. Hana maji. Hana nini wala nini?”

Kwa nini jamani kutufanya hivi viongozi jamani? Maskini alipa ushuru wake ili anyanyaswe. Ng’ombe atachoka ati!
Hata kabla ya kisa hicho cha jinsi magari ya baraza la mji wa Nairobi yalivyogeuzwa vituo vya ‘kutoza wachuuzi ushuru’ hakijanitoka akilini, nikatumiwa shairi la Mkenya mmoja ambaye analilia hali ya ufisadi nchini.

Kilichoniuma zaidi kwenye shairi hili ambalo limesambaa kote ni kuwa mshairi anaomba Mola kuweka maradhi hatari ya saratani katika nyama, ili ‘wala nyama’ wafilie mbali na ‘wameza mate’ wasalie hai.

Kwa kifupi, ufisadi na uporaji wa mali nchini umeshamiri hivi kwamba wananchi wanawaombea vifo viongozi wao!

Mitandao sasa hivi gumzo ni la mabilioni kwa mabilioni ya fedha yanayoibwa kila kukicha. Majizi twayajua. Twayatetea kwa misingi ya kabila...!

Awe ni nani na nani, mwalimu, daktari, mwanahabari, mwanafunzi, mekanika, msusi, muuza mboga, mpishi, mjakazi, bawabu, yaani kila mmoja sasa hivi anaumia kwa njia moja ama nyingine kutokana na ufisadi.

Ufisadi umekuwa ndio taaluma ya kuishi nchini.

Hivi serikali ya Kenya, viongozi mbali mbali, upinzani, mashirika ya serikali na binafsi: HAMWONI MAFUTA YA MOTO YA UFISADI YAKITIRIRIKA NCHINI. Tutaula moto wa ufisadi hadi lini?

Jamani, rais dijitali Uhuru Muigai Kenyatta, fanya kitu. Uongozi mzima wa nchi – hasa taasisi husika za kupambana na ufisadi – twakuombeni mfanye jambo.

Hali mbaya sana! Donda-ndugu la ufisadi latumaliza. Mashetani wamerudi. Hadi lini jamani?

Hassan mwana wa Ali ni Mhariri wa Michezo na Nahodha wa Nuruyalugha (RADIO MAISHA).
alikauleni@gmail.com, akaulen2@standardmedia.co.ke,
FB: Ali Hassan Kauleni, Hassan mwana wa Ali,
Twitter: @alikauleni