Kupanuliwa kwa matawi ya vyuo vikuu nchini bila kuboresha miundo-msingi kumeathiri pakubwa elimu ya juu nchini. Wataalamu katika sekta hiyo wanasema kuna haja ya serikali kuhakikisha kuwa viwango vya elimu vinavyotolewa katika vyuo vikuu nchini ni vya hali ya juu na vinaafikia viwango vya kimataifa. Akizungumza katika hafla iliyofanyika jana jioni katika chuo kikuu cha Daystar katika Msururu wa Makongamano ya Transform Kenya, Naibu Mkuu wa Chuo hicho, Laban Ayiro amesema wanafunzi wanaohitimu kutoka vyuo vikuu vya humu nchini wamesalia nyuma kutokana na viwango vya masomo vinavyotolewa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Wahadhiri nchini, Constantine Wasonga amelalamika kwamba hawahusishwi katika maamuzi muhimu ya vyuo. Ameishtumu Tume ya Elimu ya Juu, CUE kwa kuweka vikwanzo kwa wahadhiri hasa kuhusu viwango vyao vya masomo, huku akisema hakuna mpangilio wa masomo hasa katika vyuo vikuu vya umma.
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri, KUPPET Akello Misori aidha ameeleza umuhimu wa kuwapa ushauri nasaha wanafunzi ili kuwaepusha na tabia potovu.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Habari la Standard, Orlando Lyomu ameeleza kujitolea kwa shirika hili kufanikisha elimu bora nchini na kuwakuza wanafunzi ambao watakuwa na mchango muhimu katika jamii.
Makongamano ya Transform Kenya yamekuwa yakiendelezwa kwa msururu na baadhi ya mada ambazo zimeangaziwa awali ni utoshelezo wa chakula na uhifadhi wa mazingira. Shirika la Standard ni mshirika mkuu katika ajenda hiyo ya Tranform Kenya hasa katika kutumia vyombo vyake kuendeleza mjadala.