Wanafunzi kadhaa wa Shule ya Kitaifa ya Wasichana ya Nyabururu Kaunti ya Kisii wamelazwa katika hospitali mbalimbali baada ya kula chakula chenye sumu.  Hata hivyo baadhi wametibiwa na kuruhusiwa kuondoka.

Baadhi ya wanafunzi ambao hawakutaka watajwe wamesema walionywa dhidi ya kuwaeleza wazazi wao, la si hivyo wangeadhibiwa wakati wangefika shuleni na kwamba shule ingegharamia matibabu yao. 

Afisa mmoja wa afya  wa hospitali ya Nyangena ambaye pia hakutaja kutajwa amesema jumla ya wanafunzi ishirini wametibiwa tangu walipowasilishwa Alhamisi. Amesema wamebaini kuwa waliokuwa wakiugua walikula chakula ambacho hakikuwa salama.

Hata hivyo baadhi ya watetezi wa haki za binadamu kwenye Kaunti ya Kisii wakiongozwa na Eznas Nyaramba wameukosoa usimamizi wa shule hiyo kwa kutowaarifu wazazi kuhusu afya za wanao. Nyaramba aidha amewalaumu wakuu wa elimu kwenye kaunti kwa kushrikiana na wakuu wa shule kuficha ukweli kutoka kwa wazazi.

Mwakilishi wa wadi maalum wa Kaunti ya kisii anayesimamia elimu Joyce Ombasa ameishtumu vikali shuel hiyo huku akitaka wazazi kuruhusiwa kuwapeleka wanao hospitalini kwa matibabu zaidi.

Hayo yanajiri huku baadhi ya wazazi wakidai kunyimwa nafasi kuwaona wanao shuleni walipoarifiw akuhusu kisa hicho. Evans Bosire ni mmoja wa Wazazi hao.


Walioshuhudiwa wakiwamo wahudumu wa bodaboda wamekiri kuona idadi kubwa ya wanafunzi wakisafirishwa kuelekea hospitali mbalimbali mjini Kisii kuanzia Alhamisi.

Hata hivyo juhudi za kutafuta kauli kutoka kwa usimamizi wa shule zimeambulia patupu kwani hawaruhusu yeyote kuingia shuleni.