Zikiwa zimesalia takribani siku kumi na saba kabla ya kuanza kwa mitihani ya kitaifa, washikadau wa sekta ya elimu kesho watafanya mkutano kujadili namna ya kuzuia udanganyifu katika mitihani hiyo, hasa ile ya Kidato cha Nne KCSE. Mkutano huo utaongozwa na Waziri wa Elimu Amina Mohammed na utahudhuriwa na zaidi ya maafisa elfu moja.

Maafisa wanaotarajiwa katika mkutano huo ni manaibu kamishna wa Kaunti, ambao pia watapokezwa vifunguo vya makonteina mia nne hamsini na tisa yanayohifadhi karatasi za mitihani katika sehemu mbalimbali nchini. Maafisa hao pekee ndio wanaojukumiwa kufungua kontena hizo na kuzifunga wakati mitihani hiyo itakapoanza.

Wengine watakaohudhuria ni maafisa wa Tume ya Huduma za Walimu TSC na wale wa Baraza la Mitihani Nchini KNEC. Aidha Mitihani hiyo inatarajiwa kuwasilishwa mapema kwa wakuu wa elimu kwenye kaunti mbalimbali ili kuhakikisha nakala zote  zipo kabla ya kuanza kwa mitihani yenyewe.

Mbali na Amina, Waziri Fred Matiang'i wa Masuala ya Ndani ya nchi na Joe Mucheru wa Teknolojia na mawasiliano watahudhuria mkutano huo.

Suala jingine litakaloangaziwa wakati wa mkutano huo ni usalama wa walimu na watahiniwa hasa katika maeneo ya Kaskazini Mashariki.  Aidha madai kwamba zipo shinikizo kwa walimu kufanikisha udanganyifu wakati wa mitihani hiyo yatajadiliwa.

Watahiniwa takriban milioni moja, elfu mia sita, mia saba na watatu wataufanywa mtihani wa darasa la nane KCPE huku wengine elfu mia sita sitini na nne, mia tano themanini na watano wakifanya KCSE.