Rais William Ruto amehidi kutathmini upya sheria ya ubinafsishaji wa biashara chini ya kipindi cha siku 100 akiwa ofisini, kama njia mojawapo ya mbinu za kuwavutia wawekezaji.

Katika mabadiliko hayo, Rais Ruto amesema kampuni 10 za uwekezaji zitaorodheshwa katika Soko la Hisa katika kipindi cha miezi 12 pekee.

Rais amezungumza wakati wa uzinduzi wa Soko la Hisa Mtaani wa Westlands ambapo ametoa hakikisho kuwa uongozi wake umeweka mikakati ya kushirikiano na mashirika ya kifedha na taasisi mbalimbali kuwahamasisha Wakenya wa mapato ya chini.

Kwa mujibu wa Ruto mpango huo utawafanya kipaumble wahudumu wa bodaboda na mama mboga kwa kuwa ndoto yake ni kuwapa changamoto Wakenya kukumbatia mbinu za kujipatia fedha ukiwamo uwekezaji wa hisa.

Iwapo mpango huo utafanikishwa, basi uchumi wa nchini utaimarika na Wakenya kupewa uwezo wa kiuchumi kujiendeleza kupitia ushirikiano.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soko la Hisa, NSE Kiprono Kittony, amesema watashirikiana na vyombo vya habari na mashirika mengine kuwahamasisha Wakenya kuhusu nafasi mbalimbali za kujiendeleza kiuchumi.

Shughuli hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo wale wa Mamlaka ya Mtaji, Naibu wa Rais Rigathi Gachagua miongoni mwa wengine lengo likiwa kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wadogo wanapewa uwezo wa kiuchumi kujisimamia.