Rais Uhuru Kenyatta ameanzisha rasmi wiki ya maombolezo kwa ajili ya Hayati Mwai Kibaki, baada ya kuongoza hafla ya kuutizama mwili wake katika Majengo ya Bunge.

Wananchi wamepewa nafasi ya kuutizama mwili huo baada ya Kenyatta kuwa wa kwanza mapema Jumatatu.

Msafara wa Kenyatta uliwasili saa nne na dakika nne katika majengo ya bunge, muda mfupi tu baada ya Naibu wa Rais William Ruto kuwasili saa tatu na nusu jinsi ilivyopangwa na Kamati-Andalizi ya Mazishi ya Kibaki.

Kabla ya Rais ambaye alikuwa amehuzunika kuutizama mwili huo, maombi maalumu yalifanywa na makasisi wa kijeshi kisha kuelekezwa na Maafisa wa KDF akiwa na mkewe Bi. Margret Kenyatta, ambapo baadaye alipiga picha ya pamoja na wanafamilia wa Kibaki.

Aidha, George Nderitu ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Rais katika Idara ya Jeshi, na ambaye aliandama na Rais Kenyatta wakati wa kuutizama mwili huo, alipiga saluti mbili kuashiria ishara ya heshima za mwisho kwa Kibaki.

Naibu wa Rais William Ruto alikuwa wa pili kuutizama mwili wa Kibaki ambao ulitolewa Jumatatu mapema kutoka Hifadhi ya Maiti ya Lee Funeral, kabla ya makamanda wa huduma maalumu za jeshi.

Waliofuata ni maspika Justin Muturi wa Bunge la Kitaifa na Ken Lusaka wa Seneti, kisha Jaji Mkuu Martha Koome.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alifuata, baadaye mawaziri mbalimbali wakapewa fursa ya kuutizama mwili huo wa Kibaki.

Mwili wa Kibaki unalindwa na maafisa wawili ambao wamesimama kando yake; mmoja upande wa kike na mwingine wa kiume.

Ibada ya Kitaifa itafanyika Ijumaa wiki hii kabla ya mazishi ambayo yameratibiwa kufanyika Othaya, nyumbani kwa Kibaki katika Kaunti ya Nyeri.

Rais Mstaafu Emilio Stanley Mwai Kibaki, ambaye ni Rais wa tatu wa Kenya alifariki dunia Ijumaa iliyopita.