Mwanaharakati wa mazingira, Truphena Muthoni, ameweka historia baada ya kukamilisha saa 72 mfululizo za kukumbatia miti, jaribio linalotarajiwa kuweka rekodi mpya ya dunia.
Muthoni, mwenye umri wa miaka 22, alianza safari hiyo Jumatatu, Desemba 8, 2025, nje ya Ofisi ya Gavana wa Nyeri, akishuhudiwa na wafuasi, maafisa wa kaunti na wananchi waliovutiwa na tukio hilo adimu.
Akiwa na lengo la kuvuka rekodi yake ya awali ya saa 48 aliyoweka Februari 2025, Muthoni alisisitiza kuwa zoezi hilo si suala la kupima uwezo wa mwili pekee.
Alilitaja kama maandamano ya kimya dhidi ya ukataji miti, mwito wa kulinda misitu ya asili, na pia safari yake ya uponyaji wa kiakili kupitia kuungana na mazingira.
“Kukumbatia miti ni tiba. Dunia inakabiliwa na changamoto kubwa za afya ya akili zinazochochewa moja kwa moja na uharibifu wa mazingira,” alisema.
Katika kipindi hicho cha saa 72, Muthoni alivumilia mvua nzito, baridi kali, maumivu na uchovu mkali bila kula, kunywa au kupumzika, huku mikono yake ikiwa imekumbatia mti mmoja kwa uaminifu wa hali ya juu.
Ili kumpa nguvu ya kuendelea, wanaharakati wenzake waliandaa orodha maalum ya muziki inayochezwa kwa zamu, ikijumuisha mseto wa mitindo mbalimbali ya muziki ili kuweka ari, hisia thabiti na mazingira yenye uhai kadri muda ulivyosonga.
Jitihada zake zimevutia uungaji mkono mpana kutoka kwa wakazi, wanaharakati wa mazingira na viongozi wa ngazi za juu.
Aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, ni miongoni mwa waliomtia moyo hadharani, akimsifu kwa ujasiri na uthabiti.
“Truphena Muthoni, endelea binti yangu,” alisema Rigathi.
“Nakutia moyo katika dhamira yako ya kuhifadhi mazingira, sio tu kwa kuvunja rekodi ya dunia bali pia kwa kuongeza ufahamu kuhusu uhifadhi wa misitu na changamoto za afya ya akili.”
Gachagua aliongeza kuwa juhudi zake ni ukumbusho thabiti kwamba dunia inahitaji kutafakari upya kuhusu namna tunavyotunza mazingira na afya ya akili ya jamii.
Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga na naibu wake, Kinaniri Waroe, pia walifika kushuhudia, huku Gavana akielezea mshangao na fahari yake.
“Hii ni ya kipekee na ya kuhamasisha,” alisema baada ya kuona uthabiti wake.
Gavana Kahiga ndiye aliyefungua rasmi kuanza kwa kuhesabu muda wa jaribio hilo Jumatatu, akimsifu Muthoni kwa kujitolea na moyo wake wa kutetea mazingira.