NASA kuandaa maandamano makubwa Desemba
Geoffrey Mung'ou
Magavana waliochaguliwa kupitia vyama tanzu vya Muungano wa NASA, leo hii wameidhinisha mpango wa muungano huo wa kubuniwa kwa Barara za Wananchi, People's Assembly kwa lengo la kutathmini katiba na njia za kuimarisha ugatuzi. Viongozi hao wameafikiana kuwasilisha yatakayoafikiwa na baraza hilo hadi mabunge ya kaunti ya kuidhinishaji na kuwaalika viongozi wengine wa mashinani katika vikao vya baraza hilo.
Baraza hilo la wananchi litawajumuisha magavana, maseneta, wabunge, wawakilishi wadi, viongozi wa mashirika ya kijamii, kidini, wafanyabiashara na wawakilishi wa wanawake na vijana. Katika kikao kilichohudhuriwa na Raila Odinga, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula, imeafikiwa kuwa kongamano kuu litafanyika baadaye jijini Nairobi ili kujadili marekebisho ya katiba kwa lengo la kuafikia masuala mbambali kama vile: kulinda ugatuzi, kujadili muundo wa serikali tendaji yaani executive na bunge, ugavi sawa wa rasilmali, kutathmini utendakazi wa vitengo vya usalama, mageuzi katika tume ya uchaguzi na mazingira bora ya ukuaji wa uchumi.
Wakati huo huo, Muungano wa NASA umepanga kutatiza utendakazi wa serikali ya Jubilee kupitia maandamano makubwa yatakayowahusisha takribani watu milioni moja jijini Nairobi mapema mwezi ujao. Ili kufanikisha lengo hilo, kila mbunge wa upinzani atahitajika kuwasafirisha wafuasi wasiopungua elfu tatu wa NASA hadi Nairobi, kutoka maeneo bunge yao kwa ushirikiano na wawakilishi wa wadi ili kushiriki maandamano hayo ambayo yatakuwa makubwa kuwahi kufanyika. Afisa Mkuu Mtendaji wa NASA, Norman Magaya, ameiambia Radio Maisha kuwa mpango huo ni wa kuhakikisha kuwa serikali inatii matakwa ya mrengo huo yakiwamo mazungumzo na kuandaliwa kwa uchaguzi mwingine katika kipindi cha siku tisini. Aidha wanalenga kuiondoa mamlakani serikali ya Jubilee.
Kilele cha maandamnao hayo kitakuwa kuzinduliwa ramsi kwa Baraza la Wananchi. Tayari mrengo huo umebuni kamati itakayowashughulikia waandamanaji kuanzia jinsi watakavyosafirishwa hadi Nairobi na kurejeshwa baada ya maandamano, mpango wa kuwapa chakula na mahali watakapoishi katika kipindi chote cha maandamnao hayo. Aidha kamati hiyo inakagua orodha ya kampuni ambazo zinahusishwa na serikali, ili wafuasi wake washauriwe kususia bidhaa na huduma za kampuni zinazohusika.
Wakati wa maandamano hayo, NASA itakuwa na watu maalumu ambao watawaongoza waandamanaji kwa amani. Ingawa Magaya hajafichua ni siku ngapi maandamnao hayo yatadumu, inaaminika kuwa huenda yakazidi siku tatu. NASA hivyo basi imesitisha maandamano yake hadi mapema mwezi ujao, ili kuwapa nafasi watahiniwa wa mitihani ya kitaifa kabla ya kurejelea maandamano hayo mwezi ujao. Ikumbukwe wiki iliyopita, NASA ilibuni kitengo cha Kitaifa cha Vuguvugu la Mageuzi kwa lengo la kushinikiza mageuzi nchini.
NASA kuandaa maandamano makubwa Desemba
By
| Nov. 2, 2017