Familia ya Rais Mstaafu Daniel arap Moi , imewashukuru Viongozi Wakenya na Marafiki zao kufuatia jumbe za risala za rambirambi baada ya kifo cha Jonathan Moi, mwanawe wa kwanza wa Rais huyo mstaafu.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari,  familia ya Moi imesema, jumbe nyingi zimetumwa kufuatia kifo cha Jonathan hapo jana.

Familia imemtaja Marehemu kuwa mtu aliyependa kutangamana na watu na asiyekuwa na majivuno, huku ikitoa wito wa Wakenya kuipa muda wa kuomboleza ,  ikiahidi kutoa taarifa zaidi kuhusu mipango itakayoendelea baada ya kifo chake. Katibu wa Mawasiliano, Lee Njiru aidha alisema taarifa kuhusu maandalizi ya mazishi itatolewa baadaye.

Jonathan Toroitich Moi aliyezaliwa tarehe 23 mwezi Julai mwaka wa 1954,  amefariki dunia akiwa na umri wa miaka sitini na mitatu.