Maafisa wa idara ya upelelezi leo hii wanatarajiwa kuendeleza misako zaidi ya kuwanasa washukiwa wa ugaidi waliohusika katika uvamizi eneo la 14 Riverside Drive ambako watu 21 waliuliwa na wengine 28 wakiachwa na majeraha. Kufikia sasa washukiwa tisa wamekamatwa. Miongoni mwa washukiwa hao ni Ali Salim Gichunge ambaye ni mwanawe afisa wa jeshi la KDF. Awali ilirotiwa kwamba Gichunge alikuwa miongoni mwa waliouliwa katika Hoteli ya DusitD2 japo baadaye ikabainika siye.
Mkewe Gichunge, Violet Kemunto aidha anaripotiwa kutoweka tangu kushuhudiwa kwa tukio hilo japo mamaye mshukiwa ni miongoni mwa waliokamatwa. Wakazi wa eneo la Majengo Nyeri, wamezungumzia kumfahamu Gichunge ambaye aliyezaliwa na kulelewa eneo hilo. Wakazi wamemtaja kuwa kijana mtulivu hadi alipohama eneo hilo zaidi ya miaka mitatu iliyopita.
Inadaiwa washukiwa walilala nyumbani kwa Gichunge eneo la Muchatha, Kiambu na uchunguzi umebainisha kuwa alikuwa akiwasiliana mara kwa mara na washukiwa hao walioivamia Hoteli ya DusitD2. Aidha imebainika alikuwa akiwasiliana na mshukiwa mwingine kwa jina Erick Kinyanjui ambaye anaaminika kuwa kamanda wa shambulio hilo. Polisi jana walielekea nyumbani kwa kina Kinyanjui eneo la Ngecha Kiambu lakini wakaarifiwa kwamba wazazi wake walikuwa wamehamia eneo la Riara.
Washukiwa wengine walikamatwa katika Mtaa wa Ushirika, Nairobi, Kaimosi na Isiolo. Aidha maafisa wa upelelezi waliendeleza uchunguzi hadi kwenye Kaunti ya Mombasa eneo la Bondeni ambako mshukiwa mmoja mwanamke aliaminika kuwapo.
Hata hivyo mshukiwa huyo kwa jina Miriam Abdi ambaye anaaminika kusafirisha silaha zilizotumiwa kwenye shambulio hilo hakupatikana nyumbani kwake. Inaarifiwa alisafiri hadi Mombasa kutoka Nairobi siku ya Jumapili lakini hakuonekana nyumbani kwake tangu arejee.
Aidha inaaminika alikuwa na cheti bandia cha kuishi humu nchini kwani alikuwa raia wa Somalia. Polisi wangali wanamsaka mwanamume mwingine ambaye alionekana akila chakula cha mchana na washukiwa wa shambulio hilo kabla ya kutekeleza shambulio.