Huku Wakristo wakisherehekea Pasaka, kundi la waumuni wa dhehebu ya Kihindu liitwalo, International Society for Krishna Consciousness, ISKCON, linaadhimisha sherehe za kuwabeba miungu wao kwenye vijigari vinavyosukumwa kwa farasi huku waumini wa dini hiyo mjini Eldoret, wakitarajiwa kumpokea mungu wao Jaganath ambaye atasafirishwa kutoka India na makuhani wakuu msimu huu.   Ratha Yatra ama Rathajata, ni msimu wa sherehe za kuwabeba miungu kwenye misafara barabani katika dini ya Kihindu, ambapo waumini wa dini hiyo huzibeba sanamu, ishara ya ziara ya miungu duniani.

Waumini wa dini hiyo nchini Kenya wanatarajiwa kuipokea sanamu ya mungu wao mkuu maarufu Jaganath, kwa mara ya kwanza mjini Eldoret ambaye atasafirishwa kwa ndege kutoka makao yake makuu mjini Odisha - India. Partha Prema Das ni kuhani wa ISKCON.

Msafara huo huashiria dhana kwamba mungu wao Jaganath ameshuka kutoka mbinguni katika himaya yake takatifu, na kuja kutangamana na viumbe wake kwa siku hiyo kila mwaka.

Kusafirishwa kwa mungu Jaganath kuja nchini Kenya hakuna uhusiano wowote na matukio ya kisiasa bali ni ishara ya kuendeleza uhusiano baina ya miungu na viumbe kwa mujibu wa dini hiyo.

Sanamu ya mungu Jaganath kwa jina Vishnu Avatar, inatarajiwa kuhifadhiwa chini ya ulinzi mkali katika Hekalu ya Sri Ram Mandir iliyoko karibu na hospitali ya St. Luke's mjini Eldoret ambapo sanamu hiyo itaandamana na ile ya kakaye Balabhadra na dadaye Subhadra.

Waumini wa dini hiyo huadhimisha siku hiyo sambamba na kwenye mataifa mbalimbali duniani yakiwamo India, Naijeria, Uganda, Malawi na Botswana huku hafla ya kumpokea mungu Jaganath ikitarajiwa kufanyika katika ukumbi wa M.V Patel.

Sherehe hizo huandamwa na shamrashamra za mlo huku waumini wake wakitakiwa kutoa misaada ya chakula na dawa kwa maskini wakiwamo watu wenye ulemavu, wajane na mayatima.

Nchini Kenya sherehe hizo zimekuwa zikifanyika mjini Nairobi, Nakuru na Kisumu huku mji wa Eldoret ukitarajiwa kuwa wa kipekee kwa kuipokea sanamu hiyo.
Mungu huyo, Jaganath wa Kihindu atawasili rasmi nchini Jumamosi huku sherehe zikifanyika siku ya Jumapili.