Nyoyo zetu zatokota, kwa uchungu tunalia

Hisia zetu zazorota, kwa maombolezo mtawalia

Kila kukicha twashituka, kwa habari za tanzia

Kwa majonzi tumechoka, wakenya twaangamia

 

Nchi yetu ya Kenya, tukufu na ya kifahari

Tumejivunia kuwa wakenya, tumelienzi taifa letu kwa ari

Sasa twavumilia kuwa Wakenya, kwa kukosa imani na shari

Ukosefu wa usalama Kenya, umesababisha vifo vya wanahari

 

Majanga na mauaji, yamepata makao nchini

Ugaidi na ubakaji, umekita kambi mashinani

Tokea Garissa kaskazini, hadi mpeketoni kusini

Vijijini na mijini, kote kote hakuna Amani

 

Ni wapi tutaenda, tumkimbilie nani?

Wa polisi kamanda, Wakenya tufanyeni?

Rais wa Jamhuri, hadi lini jamani?

Wachanga wenda kwenye kaburi, wauawa kihayawani.

 

Ajali mabarabarani, zatumaliza kukicha

Ufisadi maafisini, zatukosesha kazi

Ukabila mashinani, ni vita kila mara

Ugaidi umeingia vyuoni, wanafunzi wauawa ovyo

 

 

Tutalia hadi lini, swali langu nauliza

Wanafunzi masomoni, bila makosa kuangamiza

La kusikitisha serikalini, ni idadi kugeuza

Na kupuuza ilani, kwa maafisa wa usalama

 

Hadi tama nimefika, kwa sala kuhitimisha

Roho zao akina kaka, maulana azilaze pema

Familia zao kwa hakika, Mterehemezi awape rehema

Na ya Kenya serikali, tambueni Wakenya TUMECHOKA!