Nomino ni majina yanayotaja mtu, kitu, mahali, jambo au hali fulani. Kabla ya kulidadavua suala la miundo ya nomino ambata, kwanza tufahamu aina zifuatazo za nomino katika lugha ya Kiswahili:
Nomino za pekee/maalumu/mahususi
Ni nomino zinazotaja kitu chenye upekee wa kuwa kimoja tu kama vile majina ya watu, nchi na mito (Zamzam, Kenya na Mto Tana).
Nomino za kawaida
Ni majina ya vitu visivyo maalumu au vya pekee kama vile kitabu, dawa na gari.
Nomino za dhahania
Zinahusu vitu vya kufikirika tu; visivyo na maumbo yanayoonekana wala kugusika mfano uchoyo na uhondo.
Nomino za jamii/ makundi
Huhusu vitu vilivyo katika makundi; visivyotokea kimoja kimoja bali katika kundi lenye vitu vingi, mfano jeshi la wanahewa na baraza la wazee.
Nomino za wingi/ tungamo
Ni majina ya vitu vilivyo katika hali ya wingi tu na visivyohesabika kama vile mafuta, sukari na manukato.
Nomino za kitenzi-jina
Huundwa kwa kupachika kiambishi ‘ku-’ mwanzoni pa vitenzi. Mifano ni kulima na kucheka.
Nomino za mkato
Huwa vifupisho vya majina ya mahusiano au umilikaji. Mifano ni mamaye (mama yake) na nduguye (ndugu yake).
Aidha, zipo nomino za udogo zinazotokana na zile za wastani ambazo hugeuzwa katika hali ya udogo kama vile kigoma na kijito, vilevile nomino za ukubwa kama vile jizi na gozi.
Miundo ya Nomino Ambata
Nomino ambata ni zile zinazoundwa kwa kuyaambatanisha maneno mawili au zaidi. Nomino za aina hii huandikwa likiwa neno moja, mfano kitozamachozi. Vilevile, huweza kutenganishwa kwa vistari vifupi, mfano isimu-jamii. Nomino ambata zina miundo ifuatavyo:
Ø Nomino na nomino. Hizi ni nomimo ambata zinazotokea kwa kuunganisha nomino mbili. Mifano ya nomino hizi ni gugumaji (gugu+maji), batamzinga (bata+mzinga), mbwamwitu (mbwa+mwitu) na askarikanga (askari+kanga).
Ø Nomino zaidi ya mbili. Nomino ambata zinazoundwa kwa kuunganisha nomino zaidi ya mbili ni kama vile mwanaelimusiha (mwana+elimu+siha) na mwanasarufimuundo (mwana+sarufi+muundo).
Ø Nomino na kitenzi. Mifano ya nomino ambata zinazoundwa kwa kuunganisha nomino na kitenzi ni bongolala (bongo+lala), hatimiliki (hati+miliki) na mamapima (mama-pima).
Ø Nomino na kivumishi. Huundwa kwa kuunganisha nomino na kivumishi. Mifano ni pembetatu (pembe+tatu), duaradufu (duara+dufu), malighafi (mali+ghafi) na mjamzito (mja+mzito).
Ø Nomino na kielezi. Mfano, kipaumbele (kipau+mbele, kipewacho umbele).
Ø Kitenzi na nomino. Mfano, chemshabongo (chemsha+bongo).
Ø Kitenzi na kitenzi. Mifano ni pandashuka (panda+shuka) na patashika (pata+shika).Ø Kitenzi na nomino. Mfano, chemshabongo (chemsha+bongo).
Ø Kitenzi na kitenzi. Mifano ni pandashuka (panda+shuka) na patashika (pata+shika).
Dibaji za Guru Ustadh, Wallah Bin Wallah
1. Akufaaye, kufa naye.
2. Mwenye wivu hutaka kupishwa njia hata kama ni jangwani!
3. Wingi wa maneno si wingi wa hoja.
4. Simba hutisha hata kama amelala au amenyeshewa.
5. Usimtekenye punda ukiwa upande wake wa nyuma.
Maneeeeeno hayo!