Bilionea wa Uturuki Elsek Osman na mwenzake Gokmen Sandikci. [Robert Menza, Standard]

Mahakama mjini Mombasa imeamuru bilionea wa Uturuki Elsek Osman na mwenzake Gokmen Sandikci kuzuiliwa kwa siku kumi na nne huku uchunguzi ukiendelea kuhusu madai ya kufadhili ugaidi yanayowakabili.

Hakimu Mkazi David Odhiambo amesema kuwa kesi inayowakabili wawili hao ni nyeti kwa sababu inahusu usalama wa taifa.

Ameongeza kuwa serikali imewasilisha ushahidi mzito chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi, POTA.

Hakimu Odhiambo pia ameagiza kuwa washukiwa hao wapewe huduma ya matibabu endapo watahitaji, pamoja na kuruhusiwa kuwasiliana na mawakili wao kabla ya kurejeshwa mahakamani tarehe ishirini na saba mwezi huu wa Januari.

Elsek Osman, ambaye ni mkimbizi wa Uturuki, alikamatwa Januari kumi na tatu katika eneo la Mtwapa, Kaunti ya Kilifi, kufuatia kisa cha ghasia za barabarani kilichohusisha gari lake aina ya V8 na msafara uliokuwa ukimsafirisha Gavana wa Wajir pamoja na Afisa Mwandamizi wa Kaunti ya Kilifi.

Mawakili wa Osman, wakiongozwa na John Khaminwa na Cliff Ombeta, wamesema kuwa mteja wao anatuhumiwa kwa madai mazito ya kufadhili ugaidi ilhali ni mkimbizi ambaye amekuwa akiishi nchini Kenya kwa zaidi ya miaka ishirini.

Wakili Khaminwa ameiambia mahakama kuwa Osman ana uwekezaji unaokadiriwa kufikia shilingi bilioni sita nchini Kenya na pia anafadhili zaidi ya wanafunzi mia tatu kwa kuwalipia karo.

Imeelezwa kuwa Osman aliingia nchini kama mkimbizi baada ya kutofautiana na Serikali ya Uturuki, hali iliyomlazimu kutafuta hifadhi nchini Kenya.