Mwaliko wa Rais William Ruto kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 20 ya chama cha ODM mjini Mombasa, umeibua hisia kwamba huenda kuna makubaliano ya kisiasa yanayochipuka.
Ruto anatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo muhimu mwishoni mwa wiki hii.
Ruto, ambaye zamani alikuwa mwanachama wa ‘Pentagon’ ya ODM, ataungana na familia ya chama hicho katika mkusanyiko wake wa kwanza wa kitaifa tangu kufariki kwa kiongozi wake mwanzilishi, Hayati Raila Odinga.
Sherehe hizo zinafanyika kwa heshima ya Raila, ambaye alitarajiwa kuongoza hafla hiyo kabla ya kifo chake cha ghafla mnamo Jumatano, Oktoba tarehe 15.
Ushiriki wa Ruto ulithibitishwa awali na Kaimu Kiongozi wa ODM ambaye pia ni Seneta wa Siaya, Oburu Odinga. Mkurugenzi Mtendaji wa ODM, Oduor Ong’wen, alisema uamuzi wa kumualika Ruto ulitokana na matakwa ya Raila kwamba waanzilishi wote wa chama wawepo katika maadhimisho hayo.
Mchambuzi wa siasa Samuel Owida anasema Ruto anaanza kujitanua upya kisiasa kupitia ODM kwa sababu idadi yake ya kisiasa imepungua na muungano wa upinzani ni tishio kubwa kwake.
“Sio kwa sababu ana upendo maalum kwa chama cha Chungwa. Changamoto anazokabiliana nazo kwa sasa kuhusu idadi ya wafuasi wake kimkakati zimemlazimisha kutafuta njia ya kujihakikishia muhula wa pili kwa vyovyote vile,” alisema Owida.
Owida aliongeza kuwa rais Ruto, ambaye anatafuta kuchaguliwa tena mwaka 2027, yupo tayari kupambana hadi mwisho, hata kama itabidi kupeperusha bendera ya ODM iwapo ndio chombo pekee kitakachomfikisha ushindi.
Waanzilishi wengine walioalikwa ni pamoja na aliyekuwa Waziri Najib Balala, huku ushiriki wa Musalia Mudavadi na Charity Ngilu ukiwa bado haujathibitishwa.
Rais wa zamani wa ODM, Uhuru Kenyatta, aliyekuwa Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka, na aliyekuwa Naibu Waziri Julia Ojiambo pia wamealikwa.
Kwa mujibu wa wakili na mchambuzi wa siasa WillIs Otieno, ambaye ni afisa mwandamizi wa chama cha Safina-Kenya, Ruto anaonekana kutafuta kuirithi ngome ya kisiasa ya Raila Odinga.
“Bila msingi wa kisiasa wa Raila, Ruto hana nafasi kubwa ya ushindi. Lakini hata akifanikiwa kuupata, bado ushindi si hakika. Kwa sasa, ODM ndicho chombo cha kisiasa alichokichagua Ruto. Atakipa kipaumbele zaidi kuliko UDA, ambacho kimepoteza mvuto kwa wananchi,” alisema Otieno.
Ushiriki wa Ruto unatarajiwa kuwa na athari kubwa kisiasa, huku uwezekano wa ushirikiano wa ODM na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 zikitarajiwa kuwa ajenda kuu katika maadhimisho hayo.
Kwa Ruto, mkutano huo utakuwa kipimo cha uungwaji mkono wake miongoni mwa wafuasi wa Raila, wakati uvumi ukizidi kuhusu nia yake ya kutaka kukidhibiti chama cha ODM katika enzi ya baada ya Raila. Ripoti za migawanyiko ya ndani ya ODM pia zimezidi kuchochea mjadala kuhusu mustakabali wa chama hicho.
Wakili na mchambuzi wa siasa, Ambrose Weda, anasema mustakabali wa ODM utategemea hatua za viongozi wake.
“Rais Ruto anajikita katika umoja na ustawi wa Kenya, pamoja na azma yake ya kuchaguliwa tena mwaka 2027. Iwapo ODM itadumu au itayeyuka, itategemea jinsi viongozi wake watakavyokumbatia wananchi na kushirikiana na rais,” alisema Weda.
Kulingana na ratiba iliyotolewa na ODM, hafla itaanza Alhamisi, Novemba 13, kwa kikao maalum cha Baraza Kuu la Kitaifa (NGC).