Kenya imepiga kengele ya tahadhari kuhusu kuongezeka kwa visa vya usafirishaji haramu wa raia wake kuelekea Asia ya Kusini Mashariki, ikilitaja eneo hilo kama tishio ambako watu wanaotafuta ajira wanadanganywa na kuishia katika mitandao ya ulaghai wa mtandaoni na ajira za kulazimishwa.
Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, alisema takribani Wakenya 400 wamekumbwa na mtego huo wa mawakala wa uajiri wasio waaminifu wanaotoa ahadi za kazi zenye malipo makubwa nchini Vietnam, Urusi, Cambodia na Myanmar, lakini mwishowe hujikuta katika hali aliyoielezea kama “aina ya utumwa wa kisasa.”
“Ni tishio lililopangwa kwa ustadi. Raia wetu huvutwa na matangazo ya ajira bandia na mawakala wanaodai kuwa katika nchi kama Thailand, kisha husafirishwa kwenda Asia ya Kusini Mashariki kwa ajili ya unyonyaji, ikiwemo ajira za kulazimishwa, ulaghai wa mtandaoni, biashara haramu ya sarafu za kidijitali, na hata uchukuaji wa viungo vya mwili,” alisema Mudavadi.
Tangu Julai 2022, ubalozi wa Kenya ulioko Bangkok; unaohudumia pia Vietnam, Laos na Cambodia umeweza kuwaokoa na kuwarejesha nyumbani karibu wahanga 500.
Hata hivyo, Wakenya 126 bado wamekwama, wakiwemo 57 walioko Myanmar na 69 nchini Thailand, ambapo baadhi yao wanaripotiwa kushikiliwa na makundi ya waasi yenye silaha.
Waziri Mudavadi alitahadharisha kwamba baadhi ya wale waliorejeshwa, ambao walipata mafunzo ya kina katika uhalifu wa kimtandao, wanaweza kuwa tishio la usalama wa kitaifa iwapo wataanzisha shughuli za ulaghai humu nchini.
Waziri huyo alitoa wito kwa serikali, mashirika ya kijamii, na wananchi kwa jumla kuungana katika kuanzisha kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji, ili kuimarisha sheria dhidi ya usafirishaji haramu wa watu, na kuweka mipango madhubuti ya kuwasaidia waathiriwa ili waweze kuanza maisha upya wanaporejea nyumbani.
Katika juhudi za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ulinzi wa raia wake katika eneo hilo, Kenya imetangaza mpango wa kufungua ubalozi mpya mjini Hanoi, Vietnam; utakaokuwa wa nne katika Asia ya Kusini Mashariki baada ya Kuala Lumpur, Bangkok na Jakarta.
Hatua hiyo inakuja kufuatia visa kadhaa vya kibalozi vilivyotikisa hisia, ikiwemo lile la hivi karibuni ambapo mtoto mchanga Mkenya alirejeshwa kutoka Indonesia, huku mama yake akibaki gerezani akikabilana na kifungo.