Chaguzi ndogo zitakazofanyika tarehe 27 mwezi huu zinatarajiwa kuwa mchuano wa kihistoria kwa Rais William Ruto, akiwa katika harakati za kuhakikisha ana nafasi bora ya muhula wa pili mwaka 2027.
Ushindi au kushindwa katika eneobunge la Malava utaibua maswali makubwa kuhusu mustakabali wa kisiasa wa serikali ya Kenya Kwanza, hususan iwapo itabidi kuwepo na mabadiliko ya uongozi au kuendelea na usanifu wa sasa unaowapa nafasi viongozi wa Magharibi, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula.
Eneobunge la Malava, Magharibi mwa Kenya, limekuwa kitovu cha mvutano wa kisiasa, huku uchaguzi mdogo ukifuatia kifo cha mbunge Malulu Injendi. Muungano tawala wa Kenya Kwanza na ule wa Upinzani wote wamejipanga vyema, kila upande ukijipiga kifua kuonyesha kuwa mgombea wake ndiye anayestahili.
Eneo la Malava ni kipimo cha nguvu ya kisiasa. Ushindi hapa si tu ni kura za wagombea, bali ni ishara ya ni nani atakayekuwa na ushawishi mkubwa katika kisiasa ya Magharibi.
Baadhi ya wachambuzi wanasema, "Kushindwa kwa David Ndakwa wa UDA kunaweza kudhoofisha ushawishi wa Rais Ruto katika eneo la Magharibi, ikizingatiwa Malulu alikuwa mwanachama wake wa karibu."
Kanda ya Magharibi imepata nafasi nyingi serikalini ikiwemo ya Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Mambo ya Nje zinazoshikiliwa na Musalia Mudavadi, pamoja na ya Spika wa Bunge la Kitaifa inayoshikiliwa na Moses Wetang’ula.
Kulingana na mchambuzi wa siasa Herman Manyora, ushindi wa upande wa Ruto unaweza kubadilisha historia ya eneo lililosalia katika upinzani kwa muda mrefu.
"Huu si tu uchaguzi mdogo, ni kipimo cha ushawishi wa Ruto kabla ya 2027." Herman Manyora, Mchambuzi wa Siasa:
Swali kuu sasa ni, Eneo la Magharibi litaamua nini ifikapo tarehe 27?... Ikizingatiwa kuwa ushindi wa Malava unaweza kuashiria mwendo mpya wa kisiasa kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.