Picha ilioundwa na AI yaonesha pembe iliomea kwa uso wa binadamu. 

Wanyama wa familia ya farasi, wakiwemo farasi, punda na pundamilia, wanashiriki sifa ya kushangaza inayoitwa chestnuts. Hizi hupatikana kwenye miguu ya kila farasi, na huonekana kama vijivimbe vigumu vya ngozi ambavyo vinaweza kukatwa vikizidi kukua.

Watumiaji wa mtandao wa TikTok wanaomfuatilia fundi wa viatu wa farasi Sam Wolfenden watakuwa wameona ustadi wake wa kuyakata na kuyarekebisha chestnuts hizo.

Chestnuts ni mabaki ya kimaumbile ya pedi za vidole vilivyokuwepo kwa aina ya zamani ya farasi wa sasa na wa porini. Pia ni za kipekee kwa kila mnyama na zinaweza kufananishwa na alama ya vidole vya mtu.

Chestnuts hutengenezwa na keratini, dutu inayopatikana kwenye safu ya nje ya ngozi. Kazi yake ni kulinda mwili, kuzuia maji kupenya na kutoa uimara. Keratini pia hupatikana kwenye nywele na kucha, ambavyo vina jukumu la kuhifadhi joto na kutoa taarifa za hisia kwa ubongo.

Kwato za farasi na pembe za wanyama pia hutengenezwa na keratini, zikiwa na majukumu ya kulinda na hata kutumika kama silaha.

Hivyo, keratini ina umuhimu kwa binadamu na wanyama. Na kwa kuwa miili yetu imejengwa kwa misingi inayofanana, si ajabu kwamba binadamu pia wanaweza kukuza vitu vinavyofanana na pembe; ingawa si kama za mbuzi au kondoo.

Pembe za Binadamu

Cutaneous horns ni uvimbe mgumu wa keratini unaokua nje ya ngozi ya binadamu. Umbo lake hujipinda na ugumu wake huufanya uonekane kama pembe ya kozi au kondoo.

Rangi yake huanzia ya njano hadi kahawia au kijivu, kutegemea kiwango cha seli zilizokufa na rangi zilizofungamana ndani yake.

Vijivimbe hivi hutokana na mabadiliko au vidonda vya ngozi. Mara nyingi havina madhara. Aina mbalimbali za vipele vya ngozi, ikiwa ni pamoja na vinavyosababishwa na virusi vya HPV, vinaweza kusababisha pembe hizi.

Hata hivyo, kati ya asilimia 16–20 ya cutaneous horns hutokana na saratani ya ngozi, hasa squamous cell carcinoma, aina ya saratani inayoweza kuenea ikiwa haitatibiwa.

Kwa watu wengine, pembe hizi hutokana na hali zinazoelekea kuwa saratani, kama vile actinic keratosis, ambayo mara nyingine huhusiana na jua.

Uvunjifu wa muundo wa seli na ukuaji usiodhibitiwa unaweza kusababisha mkusanyiko mkubwa wa keratini na hivyo kutengeneza pembe.

Watu wanaopata pembe hizi mara nyingi ni wazee wenye ngozi nyepesi na ambao hukaa kwenye jua muda mrefu, ishara kuwa mwanga wa jua wa UV una mchango mkubwa.

Zinavyoweza Kukua Kupita Kiasi

Cutaneous horns zinaweza kujitokeza sehemu mbalimbali za mwili, hata kifuani au sehemu za siri. Kwa kuwa wakati mwingine huhusiana na saratani, mtu yeyote anayegundua uvimbe huu anapaswa kumuona daktari.

Matibabu mara nyingi ni upasuaji mdogo wa kuondoa pembe na ngozi ya pembeni mwake.

Baadhi ya pembe zimewahi kukua hadi ukubwa wa kushangaza. Mwaka 2024, mwanamke mmoja nchini China alivutia vichwa vya habari baada ya pembe kukua kwenye paji la uso wake hadi sentimita 10 katika miaka saba.

Katika karne ya 19, Madame Dimanche wa Ufaransa alikua na pembe iliyofikia karibu sentimita 25 kabla ya kuondolewa, na mfano wake wa nta bado unahifadhiwa kwenye Jumba la Makumbusho la Mütter huko Philadelphia.

Usipuuze

Ukigundua uvimbe mgumu unaofanana na pembe, hata kama ni mdogo, muone daktari kwa ushauri na tiba sahihi.

Na kwa Sam Wolfenden wa tiktok, endelea na kazi yako ya kukata kwato, itafurahisha wengi.