Chama cha Wataalam wa Uthamini na Upimaji wa Ardhi Kenya (ISK) kimesema kuwa ukataji miti ovyo, matumizi yasiyo endelevu ya ardhi na upangaji duni wa makazi vimeongeza kwa kiasi kikubwa matukio na madhara ya maporomoko ya ardhi nchini.
Kwa mujibu wa ISK, kuendelea kuharibiwa kwa misitu kumeosheleza udongo, kudhoofisha miinuko na kuvuruga mifumo ya asili ya maji ambayo husaidia kuzuia majanga kama haya.
Rais wa ISK, Erick Nyadimo, alisema Kenya imerekodi zaidi ya matukio 120 ya maporomoko ya ardhi katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, ambapo Kaunti ya Elgeyo Marakwet ni miongoni mwa kaunti tano zilizo hatarini zaidi.
Hadi sasa watu 26 wamethibitishwa kufariki baada ya maporomoko ya udongo kukumba Elgeyo Marakwet wiki iliyopita katika maeneo ya Murkutwa, Chesongoch, Kabetwa na Embobut katika Marakwet Mashariki.
Zaidi ya watu kumi hawajulikani walipo kufikia sasa, huku familia 500 zikipoteza makazi baada ya mito kufurika na kusababisha mafuriko yaliyodumu usiku kucha.
Akitoa pole kwa waathiriwa, Nyadimo aliwataka wananchi kukomesha tabia ya kukata miti kwa ajili ya kilimo, malisho, uchomaji mkaa na makazi.
“Mpango wa Serikali wa kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032 ni wa kuungwa mkono, lakini juhudi hizi lazima ziende sambamba na utekelezaji madhubuti wa mipango ya matumizi ya ardhi, uhifadhi wa mazingira na udhibiti wa makazi. Bila hivyo, lengo hilo litasalia kuwa ndoto,” alisema Nyadimo.
Aliongeza kuwa kile kilichotokea Elgeyo Marakwet ni onyo kwamba jamii zinazoishi maeneo hatari zinahitaji hatua za haraka za kitaifa kuhusu maandalizi ya kukabili majanga pamoja na matumizi endelevu ya ardhi.
Nyadimo alisema ni jambo la kusikitisha kwamba licha ya tahadhari za mapema za Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa, bado maisha yalipotea kutokana na uhamishaji duni, miundombinu hafifu na ukosefu wa maeneo rasmi ya hifadhi kwa wakazi wa maeneo hatarishi.
Nyadimo aidha alisisitiza Serikali inapaswa kushirikiana na taasisi za kitaalam kama ISK kufanya upimaji wa kijiografia ili kubaini na kufuatilia maeneo hatarishi nchini.
Aidha, mifumo ya onyo la mapema inapaswa kuunganishwa moja kwa moja na hatua za haraka za jamii ikiwa ni pamoja na uhamishaji wa watu na utoaji wa makazi ya muda.
ISK pia imependekeza urejeshwaji wa misitu na maeneo ya vyanzo vya maji kwa kuimarisha upandaji miti, kudhibiti ukataji miti na kuhimiza kilimo endelevu ili kulinda udongo na vyanzo vya maji.