Naibu Rais Kithure Kindiki akaribishwa Kaunti ya Kitui Juni 27, 2025, kwenye hafla ya kuwahamasisha wakina mama. [Philip Muasya, Standard]

Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kudai nafasi ya Naibu Rais kama sharti la kumuunga mkono Rais William Ruto katika azma yake ya kuchaguliwa tena kumesababisha mvutano mkubwa wa kisiasa ndani ya kambi ya Rais Ruto.

Washirika wa Naibu Rais Kithure Kindiki wanaripotiwa kutoridhishwa na matamshi ya Oburu Oginga, wakimwona kama anayevuruga mipango ya Kindiki ya kuwania urais mwaka 2032, endapo Ruto atashinda katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Wachambuzi wa siasa waliozungumza na Radio Maisha wamesema matamshi ya Oburu ni mazito kisiasa. Tayari, kundi la wanasiasa kutoka Meru wanaomuunga mkono Kindiki wametoa onyo kwa Rais Ruto kufuatia madai hayo ya ODM.

Wakiongozwa na Mbunge wa Tigania Magharibi John Mutunga, wabunge hao walimshukuru Rais Ruto kwa kuipa jamii ya Meru nafasi ya juu serikalini kupitia uteuzi wa Kindiki kama Naibu Rais.

Hata hivyo, waliisisitiza kuwa nafasi hiyo ya Naibu Rais inafaa kuendelea kubaki katika eneo la Mashariki ya Mlima Kenya.

Kiongozi mwandamizi wa chama cha ODM Oburu Oginga akihutubia waombolezaji katika ibaad ya wafu ya alikuwa Waziri Mkuu Raila Odinga katika uwanja wa Kimataifa wa michezo wa Nyayo Oktoba 17, 2025. [Boniface Okendo, Standard]

“Sisi watu wa Meru hatujawahi kuwa na nafasi hii kwa muda mrefu. Wanaoitaka sasa waseme wanaitaka, lakini kiti hiki ni chetu,” alisema Mutunga.

Mbunge huyo pia aliwataka viongozi wa eneo hilo kuhamasisha usajili wa wapiga kura, akisisitiza kuwa nguvu halisi ipo kwenye kura, na kwamba idadi kubwa ya wapiga kura italipa eneo la Meru ushawishi katika maamuzi ya kitaifa.

Mchambuzi wa siasa na wakili wa Mahakama Kuu Ambrose Weda alisema Oburu hana ustadi wa kisiasa na anahitaji ushauri juu ya namna ya kushughulikia masuala yenye athari pana.

“Raila hakuwahi kujadili mambo makubwa hadharani. Mazungumzo ya mambo makubwa hufanyika chini kwa chini. Oburu anahitaji ushauri wa kimkakati,” alisema Weda.

Oburu, ambaye sasa ndiye kaimu Kiongozi wa ODM kufuatia kifo cha ndugu yake, Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, alisisitiza kuwa chama hicho hakitakubali nafasi iliyo chini ya Naibu Rais.

“Ikiwa tutachukua nafasi, haitakuwa chini ya nambari mbili; Naibu Rais,” alisisitiza.

Viongozi wengine wa ODM akiwemo Gavana wa Kisii Simba Arati na Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, pia wamemtaka Rais Ruto kurejea ODM, wakipendekeza kuwa anaweza kuwa mgombea wa chama hicho katika uchaguzi wa 2027.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, ODM ipo ndani ya haki kudai sehemu kubwa ya nafasi serikalini, ikizingatiwa kuwa eneo la Mlima Kenya linaonekana kutokuwa na msimamo dhabiti kuhusu kumuunga mkono Ruto katika jaribio lake la kuchaguliwa tena.