NAIROBI, KENYA, Kwa mara nyingine tena mwanaharakati wa upinzani Miguna Miguna amefurushwa nchini. Miguna maefurushwa kwa nguvu baada ya maafisa wa polisi kuvunja lango la sehemu ya choo ambapo amekuwa akizuiliwa tangu kuwasilia katika uwanja wa JKIA siku tatu zilizopita.    Kwa mujibu wa mmoja wa maafisa wa Tume ya  Kitaifa Haki za Kibinadamu Kamanda Mucheke, maafisa hao walimchukua pindi alipoondoka kwenda kumtafutia chajio.   Maafisa hao wamemlazimu kuabiri ndege aina ya EK 722 kuelekea Dubai. Mbunge wa Gatrundu Kusini, Moses Kuria ambaye ni miongoni mwa waliokuwa katika ndege hiyo, amethibitisha kupitia mtandao wa kijamii kwamba Miguna Miguna alikuwapo. Taarifa zaidi zinaarifu kwamba huenda alitiwa pingu na kudungwa dawa ya kumtuliza kabla ya kuabirishwa ndege hiyo.   Hatua hii imechukuliwa wakati ambapo serikali imewekwa chini ya mizani ya mahakakama kwa kuendeleaa kukiuka maagizo ya mahakama la hivi punde likiwa gaizo la Jaji George Odunga kumwasilisha mahakamani. Kutokana na hatua hiyo, Jaji huyo amemwagiza Waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi, Fred Matiang'i Inspekta Mkuu wa Polisi, Joseph Boinet na Katibu Mkuu  Idara ya Uhamiaji Gordon Kihalangwa kufika makamani saa nne leo asubuhi, wakati wa kusomewa hukumu ya kukiuka maagizo ya mahakama.   Odunga ametoa uamuzi huo baada ya mawakili wa Miguna kupendekeza kifungo cha miezi sita dhidi ya watatu hao pamoja na maafisa wengine ambao wamekuwa wakimzuilia Miguna katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, JKIA tangu siku ya Jumatatu. Odunga aidha ameagiza Miguna awachiliwe huru na kuwasilishwa mahakamani Alhamisi asubuhi.   Miguna alistahili kuwasilishwa mahakamani mwendo wa saa tatu asubuhi kufuatia agizo la Jaji Rosylne Aburili siku ya Jumanne baada ya yeye kupitia mawakili wake kuishtaki serikali kwa kuendelea kuzuiliwa. Lakini hilo halikufanyika huku wakili wa Idara ya Uhamiaji, Charles Mutinda akisema Miguna hawezi kuondolewa JKIA bila kuwa na stakabadhi za kumruhusu kuwa nchini, utetezi uliopuuzwa na Jaji George Odunga.   Mawakili wa Miguna waliteta kwamba hawatakubali kuendelea kwa kesi bila kuwasilishwa kwa mteja wao, hali iliyochangia kuahirishwa kwa vikao hadi saa nane unusu baada ya kuahirishwa awali mwendo wa saa nne ili kutoa nafasi kwa wakili huyo kuwasilishwa mahakamani. Hata hivyo ilipofika adhuhuri Miguna hakuwapo huku mawakili wa upande wa utetezi, wakijitetea.   Wakili Otiende aidha amelalamikia dharau iliyodhihirishwa dhidi ya mahakama baada ya upande wa washtakiwa kuwawasilisha mawakili wasio na uzoefu wa miaka mingi kazini.    Inasubiriwa kuona sarakasi zaidi zitakazoshuhudiwa kutokana na kisanga cha Miguna hasa baada ya serikali kumfurusha tena wakili huyo.?