Mahakama ya Upeo inasubiriwa kutoa Jumatatu uamuzi kuhusu kesi ya kupinga ushindi wa Rais Mteule William Ruto.

Jopo la Majaji Saba likiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome linatarajiwa kudumisha ama kufutilia mbali ushindi wa Ruto.

Iwapo utadumishwa, basi Ruto ataapishwa Jumanne wiki ijayo ambapo Kamati ya Mpito itaendesha shughuli za maandalizi ya siku hiyo.

Aidha, ushindi huo ukifutiliwa mbali, taifa litaelekea debeni ndani ya siku 60 ambapo marudio ya uchaguzi wa urais yatafanyika Novemba tarahe 4.

Katika uamuzi huo, majaji hao watajikita zaidi katika masuala tisa yaliorodheshwa katika kikao cha utangulizi.

Kwenye uamuzi wake, jopo hilo litabaini iwapo vifaa vya kiteknojia vya Tume ya Uchaguzi, IEBC viliafikia vigezo vinavyohitajika kufanikisha usalama na uwazi katika mchakato mzima wa kupiga kura, iwapo mchakato wa kuweka fomu 34A katika wavuti wa IEBC uliingiliwa inavyodaiwa, na iwapo tume hiyo ilithibitisha matokeo kabla ya kutangazwa inavyohitajika kisheria.

Mambo mengine ni iwapo kuahirishwa kwa uchaguzi kwenye maeneo manane nchini ulitatiza idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura, iwapo Ruto aliafikia ushindi wa asilimia 50 na kura moja na kama sheria ilizingatiwa kwa ujumla wakati wa uchaguzi mkuu.

Majaji hao, Martha Koome, Philomena Mwilu, Smokin, Wanjala, Isaac lenaola, Njoki, Ndung'u, William Ouko na Mohamed Ibrahim wamekuwa katika shughuli ya kuandaa uamuzi wakendi baada ya vikao kukamilika Ijumaa.