Katibu wa Utawala katika Wizara ya Masuala ya Nje ya Nchi, Ababu Namwamba amejiuzu wadhifa huo, siku moja tu baada ya kuteuliwa kuongoza shughuli za nje ya nchi katika kampeni za urais za Naibu wa Rais, William Ruto.

Namwamba amesema atashirikiana na Kamati Kiufundi inayoshughulikia kampeni za Ruto ili kufanikisha azma ya Ruto kuwa rais Agosti 9.

Ababu atajukumiwa kuzuru mataifa mbalimbali akiyarai mataifa kuunga mkono sera za Ruto.

Ababu amemshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kumteua kuwa Katibu wa Utawala, akiahidi kushirikiana naye iwapo atapewa nafasi nyingine katika siku zijazo.

Pia Ababu ameshukuru ofisi ya Ruto kwa kumteua kuwa miongoni mwa wanaoendeleza kampeni za urais nchini na hata mataifa mengine.