Mamlaka ya Kitaifa ya Takwimu, KNBS imeelezea utayarifu wake katika kuendesha shughuli ya sensa mwezi ujao. Haya yanajiri huku shughuli ya kuwachuja waliotuma maombi ya kazi ya sensa iking'oa nanga rasmi leo hii. KNBS aidha imesema shughuli hiyo itaanza tarehe 24 mwezi Agosti na kukamilika tarehe 31 mwezi uo huo.

Mkugenzi Mkuu wa KNBS, Zachary Mwangi amesema sheria zilifuatwa wakati wa kuyaorodhesha majina ya waliotuma maombi. Shughuli ya uchujaji inatarajiwa kukamilika Ijumaa wiki hii na itafanywa kwa uwazi.

Baada ya shughuli hiyo kukamilika, watakaofanikiwa watafanyiwa mafunzo kuanzia tarehe 15 mwezi huu. Mwangi amesema takriban watu elfu mbili mia saba wa kitengo cha ICT watateuliwa huku elfu ishirini na saba wakichukuliwa katika kusimamia jinsi shughuli hiyo itakavyoendeshwa. Aidha, watu elfu 135 kwa Kimombo, enumerators watateuliwa kuendesha shughuli ya usajili wa watu, .

Mwangi amesema kila atakayeteuliwa atatumwa katika kaunti anakotoka ili kurahisisha shughuli yenyewe.

Je, wafahamu umuhimu wa sensa?

Shughuli hii hutumiwa na serikali katika mchakato wa uundaji sera.

Sensa aidha huiwezesha serikali kupata takwimu kuhusu idadi ya wanaozaliwa au kuaga dunia na ukuaji wa idadi ya watu, hivyo kupangia utoaji huduma mbalimbali.

Aidha, hutoa mwanga kuhusu idadi ya watu kulingana na umri, ambapo takwimu hizo vilevile husaidia katika mipango ya utoaji huduma.

Sensa vilevile hutoa mwanga kuhusu hali mbalimbali za mapato miongoni mwa wananchi hivyo kurahuhisha shughuli za utozaji kodi na kuamua viwango vya kodi yenywe kulingana na mapato na idadi ya watu.

Pia hutoa mwanga kuhusu jinsia, hivyo kupangia namna ya kuafikia usawa katika jamii.

Sensa pia huiwezesha nchi kufahamu idadi ya watu kulingana na makabila, takwimu zinazotumiwa katika mipangilio ya masuala mbalimbali ya kitaifa.

Aidha, idadi ya watu kulingana na maeneo hutumiwa hasa na tume ya uchaguzi na uratibu wa mipaka kuamua maeneo ya mipaka na yale ya uwakilishi.

Umuhimu mwingine wa sensa ni kujua eneo alikozaliwa mtu na anakoishi ili kufahamu mkondo wa kuhama kwa watu kutoka eneo moja hadi jingine.